Wednesday, May 11, 2016

GREEN VOICES WASAIDIA KILIMO CHA UYOGA DAR

Bi. Esther Chiombola akionyesha uyoga ambao uko tayari kuvunwa. Uyoga huo unalimwa na kikundi cha Tunza Women Group cha Bunju jijini Dar es Salaam kwa ufadhili wa mradi wa Green Voices (Makala na Picha zimeandaliwa na www.brotherdanny.com).
Bi. Sauda Issa miaka 70 (kushoto) mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam akipokea zawadi ya kitabu maalum kinachozungumzia kilimo cha uyoga kutoka kwa Bi. Esther Chiombola ambaye ni Ofisa Kilimo Msaidizi Mwandamizi wa Manispaa ya Kinondoni.
Mratibu wa vikundi vya kilimo cha uyoga Bunju na Boko, Magdalena Bukuku (katikati) akiteta jambo na mratibu wa green Voices nchini Bi. Secelela Balisidya wakati wa uzinduzi wa mradi huo unaofadhiliwa na Green Voices. Wengine pichani kutoka kushoto ni Bi. Lucresia Tarimo aliyemwakilisha Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Kinondoni, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kilungule Seif Stambuli, na Ofisa Kilimo Kata ya Bunju, Rhoda Mruttu. 
Bi. Sophia Chove, mwenyekiti wa kikundi cha wakulima wa uyoga Bunju, akitoa maelekezo kwa watu mbalimbali kuhusu namna ya uchanganyaji wa vimeng’enyo vya kuoteshea na kukuzia uyoga. 



Mchanganyiko maalum wa vimeng’enyo vinavyotumika katika kilimo cha uyoga. 



Uyoga ukiwa unaoteshwa katika eneo maalum kwa kufunikwa kaniki. 

Mchuzi mzito wa uyoga ulioandaliwa kwa ajili ya chakula cha mchana. Uyoga huo umevunwa katika mradi wa kikundi cha akinamama wa Bunju chini ya ufadhili wa Green Voices. 
Wageni waalikwa wakishiriki chakula cha mchana ambacho mboga kuu ilikuwa uyoga. 
Akinamama sita, ambao ni sehemu ya akinamama 15 ambao wanatekeleza mradi wa Green Voices baada ya kupatiwa mafunzo nchini Hispania mwanzoni mwa mwaka huu. Kutoka kushoto ni Siddy Abubakar Mgumia, Farida Hamisi, Tukuswiga Mwaisumbe, Secelela Balisidya, Magdalena Bukuku na Judica Losai.

WAKATI Magdalena Bukuku anaibua wazo la kilimo cha uyoga akiwa mafunzoni jijini Madrid, Hispania mapema mwaka huu 2016 hakutegemea kama angeweza kupata mwitikio mkubwa kutoka kwa akinamama wa maeneo ya Boko na Bunju jijini Dar es Salaam anakoishi.

Lakini leo hii, Magdalena, ambaye ni miongoni mwa akinamama 15 wanaotekeleza Mradi wa Green Voices maalum kwa kupaza sauti za wanawake kwa ajili ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, anafarijika baada ya wazo lake hilo kuzaa matunda.

Tayari wanakikundi cha ‘Tunza Women Group’ cha Bunju wameanza kuvuna kidogo kidogo uyoga ikiwa ni takriban mwezi mmoja tu tangu walipopatiwa mafunzo, huku wale wa Boko wakiwa katika hatua nzuri za kuendeleza shamba lao.

“Ni mradi mzuri, unatumia gharama kidogo huku mavuno yake yakiwa endelevu hasa ukiwa na nia, dhamira na jitihada, hapa Bunju tayari akinamama wameanza kuvuna uyoga, ambao soko lake lipo kubwa,” anaeleza Magdalena.

Magdalena ni mmoja wa akinamama wanaotekeleza kwa vitendo mradi wa Green Voices, ambao unafadhiliwa na taasisi inayojihusisha na maendeleo ya wanawake wa Afrika, ijulikanayo kama Foundation for Women of Africa inayoongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega.

Akinamama wengine wanatekeleza miradi mbalimbali ya ujasiriamali unaoendana na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kigoma, Kilimanjaro, Pwani na Mwanza.Anasema, uyoga ni zao linalohitaji eneo dogo na matumizi kidogo lakini endelevu ya rasilimali maji, hivyo kuwa rafiki mkubwa wa mazingira licha ya umuhimu wake kwa afya ya binadamu.

Uyoga ni aina ya kuvu (fungi) na hauna uwezo wa kujitengenezea chakula kama ilivyo mimea mingine ya rangi ya kijani, hivyo ili kuota na kustawi, inahitaji chakula ambacho kimekwishatengenezwa kutoka katika mimea iliyooza.

Sophia Chove, mwenyekiti wa kikundi cha ‘Tunza Women Group’ katika Mtaa wa Kilungule - Bunju, anaeleza kwamba, wamepata fursa nzuri ya kuongeza pato la familia pamoja na kushiriki katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira.

“Kikundi kina wanachama 10, lakini kwa matokeo ambayo yameonekana, wanawake wengi zaidi wamevutiwa na wanahitaji kujiunga nasi, tunaamini haya ni mafanikio na siyo vibaya kama kila kaya itaendesha kilimo hiki ambacho hakihitaji ardhi kubwa,” anasema na kupongeza hatua ya Green Voices kuwapatia mradi huo.

Kuhusu masoko, Sophia anasema uyoga ni bidhaa inayohitajika sana ambapo ikiwa watauza reja reja, kilo moja inauzwa kwa Shs. 10,000, ingawa alikiri kwamba wanahitaji kupata soko kubwa zaidi kwa vile wanataka kupanua uzalishaji wao.Akaongeza: “Tumekwishaongea na super market moja ambapo wahusika wametutaka tupeleke kwa wingi mara tutakapoanza uvunaji.”

Mradi wa Green Voices ni wa pekee nchini Tanzania kufadhiliwa na taasisi ya Foundation for Women of Africa, ambao lengo lake kubwa ni kuwasaidia akinamama kupaza sauti katika masuala ya mazingira kwa kutumia njia ya ujasiriamali.
“Mama Maria Teresa, baada ya kutoka madarakani, aliamua kuanzisha taasisi hiyo kwa nia ya kuwakomboa wanawake wa Afrika, ambao ndio waathirika wakubwa wa athari za uharibifu wa mazingira pamoja na mabadiliko ya tabianchi,” anaeleza Secelela Balisidya, Mratibu na msimamizi wa mradi huo nchini.

Secelela, ambaye kitaaluma ni mwandishi aliyejikita zaidi katika habari za mazingira, anasema ujio wa Green Voices utawakomboa wanawake wengi wa Tanzania kupitia miradi waliyoibuni ambayo itasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kama inayoelekezwa katika Malengo Endelevu ya Dunia.

Anasema, katika uhalisia, mwanamke ndiye muathirika mkubwa wa mazingira kwani anatumia muda mwingi kutafuta maji na nishati, hasa kuni, kwa ajili ya matumizi ya familia, kuliko kufanya shughuli zingine za maendeleo.

“Mradi kama huu wa kilimo cha uyoga ni rafiki wa mazingira kwa sababu hauhitaji maji mengi, lakini una faida kubwa kiafya hasa kutokana na ukweli kwamba, hivi sasa watu wengi wameathirika kwa kula vyakula vinavyozalishwa kwa kemikali,” anaongeza.

Esther Chiombola ‘Mama Uyoga’, Ofisa Kilimo Msaidizi Mwandamizi wa Manispaa ya Kinondoni ambaye ndiye aliyewafunza wanakikundi hao wa ‘Tunza Women Group’, anasema uyoga ni lishe bora ambayo imejaa kiasi cha asilimia 20 hadi 49 cha protini pamoja na Vitamini B, C, D, E, na K, na madini joto, chuma, fosforas, potashi, zinki na shaba na kwamba hauna lehemu (cholesterol).

Anasema kwamba, baadhi ya aina za uyoga kama Ganoderma husaidia kuzuia na kupunguza kasi ya magonjwa sugu kama saratani, kisukari, kifua kikuu, moyo, shinikizo la damu na figo.“Lakini ikumbukwe kwamba kilimo cha uyoga ni ajira kubwa kwa akinamama, vijana, wazee na wastaafu na ni kilimo rafiki kinachopunguza uchafuzi wa mazingira kwa vile kinatumia mabaki ya shambani na viwandani,” anafafanua.

Anataja faida nyingine kama kilimo endelevu cha mwaka mzima na kwamba mabaki yake baada ya mavuno kukoma ni mbolea nzuri na chakula cha mifugo.“Kilimo cha uyoga kinasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na kula vyakula vyenye sumu kwani mbegu zinazotumika zimefanyiwa utafiti na zinapatikana kutoka taasisi maalumu kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Kituo cha Utafiti wa Kilimo-Uyole, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Bustani Tengeru na Shirika la TIRDO,” anasema.

Bi. Chiombola anasema kwamba, aina zinazofaa kwa Tanzania ni zile ambazo hustawi vizuri, kwenye maeneo ya joto la wastani wa nyuzi joto 20C hadi 33C na kiasi cha unyevunyevu cha asilimia 75.Hata hivyo, anasema kutokana na hali ya joto la Dar es Salaam, aina inayolimwa Zaidi ni Chaza (Oyster mushroom) ambayo inastahimili hali ya joto kwa nyuzi joto 12 – 30 ambapo kundi hilo linahusisha aina ya Pleurotus sapidus (mweupe na mwingine rangi ya udongo) pamoja na Pleurotus sajor – caju.

Mahitaji muhimu ya kilimo cha uyoga yanatajwa kwamba ni banda la kuanzia ukubwa wa meta 4 kwa 5 ambalo linatosha kuotesha mifuko 450 hadi 500, vimeng’enywa ambavyo ni masalia makavu kama mabua ya mahindi, majani makavu ya mgomba na ya viwandani kama maganda ya alizeti.

Pia inahitajika mifuko maalum inayostahimili joto ambayo hutumika kujazia vimeng’enya, vifaa vya kazi kama mapipa ya kuchemshia maji, turubai la plastiki, vipete, pampu ya kumwagilia, mbegu za uyoga, vifungashio vya plastiki, visahani, virutubisho hasa pumba laini, sukari au molasses, chokaa na dawa kwa ajili ya usafi, hasa Dettol na spiriti.

Kabla ya kuanza uzalishaji ni lazima kiwepo chumba chenye paa linalozuia jua, mvua, na vumbi ambacho pia kinapaswa kiwe na sakafu inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha utando wa uyoga. 

“Baada ya hapo kuandaa masalia na mambo mengine kama utakavyoelekezwa na mtaalamu, jaza vimeng’enyo hivyo kwenye mfuko wa sandarusi wenye upana wa sm 40 - 45 na kimo cha sm 75. Weka tabaka la mali ghafi ya kuoteshea yenye kina cha sm 10 katika mfuko halafu tawanya mbegu ya uyoga juu yake. Baada ya kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya vioteshea na kuweka mbegu juu yake. Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka ifike ujazo wa robo tatu ya mfuko,” anasema Bi. Chiombola.

Anasema baada ya hapo unatakiwa kufunga mifuko na toboa matundu kwenye mifuko yenye kipenyo cha sm 1 kwa kila umbali wa sm 6 hadi 10 kwa kila mfuko ili yaweze ili kuingiza hewa ya kutosha ndani ya mifuko. 

“Weka mifuko kwenye chumba cha giza. Kwa mkulima wa kawaida waweza kutumia kasha lisilopitisha mwanga kama chumba cha giza au funika kwa kaniki. Acha mifuko humo kwa muda wa wiki tatu hadi nne bila kufunua ili ukungu mweupe uweze kutanda vizuri.

“Utando mweupe ukishatanda vizuri kwenye mali ghafi ya kuoteshea fungua mifuko, visha viringi, hamishia kwenye chumba chenye mwanga na hewa ya kutosha kisicho pigwa na jua. Mifuko inaweza kuwekwa kwenye, meza, chanja la waya au miti. Anza kumwagilia kwa pampu (mvuke wa maji baridi) na baada ya wiki moja na nusu uyoga utaanza kuchomoza,” anaeleza Bi. Chiombola. 


Bi. Chiombola anasema kwamba, uyoga huwa tayari kuchumwa siku tatu baada ya vichwa /pini kuonekana. Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika katikati ya shina la uyoga kisha zungusha hadi uyoga ung'oke. Usiondoe kichwa peke yake katika kuvuna uyoga kwani kubakiza shina huzuia uyoga mwingine kutokea. Mkulima anatakiwa ajue soko la uyoga kabla ya kuvuna ili kuepuka gharama za kuhifadhi kwani uyoga ukishavunwa unatakiwa uliwe kabla haujaharibika,” anaeleza.

Inaelezwa kwamba, uyoga ukishavunwa unaweza kuhafadhiwa kwenye jokofu kwa muda wa siku 7 kabla ya kuharibika, lakini haipaswi kuhifadhi kwenye friza.

No comments: