Wednesday, May 11, 2016

GGM na TACAIDS wamteua Mrisho Mpoto kuwa Balozi wa Kili Challenge

Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya kupambana na Ukimwi nchini (TACAIDS) imemteua msanii maarufu Mrisho Mpoto kuwa balozi wa kampeni ya Kili Challenge.

Kili Chalenge ni kampeni inayolenga kukusanya fedha kwa ajili ya kutunisha mfuko wa mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI. Kampeni hiyo ilianzishwa miaka 15 iliyopita na hufanyika kila mwaka kwa wadau mbalimbali kupanda mlima Kilimanjaro.Mwaka uliopita 2015 watu 39 walifanikiwa kupanda Mlima na kuchangisha fedha zaidi ya Sh bilioni 1.2  ambazo zitagawiwa kwa Asasi mbalimbali tarehe 20 Mwezi huu pale Hyatt Regency Dar es Salaam,Mgeni rasmi atakuwa makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Mrisho Mpoto ameteuliwa kuiwakilisha na kuitangaza kampeni hii ili kusaidiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali ndani na nje ya Tanzania kupambana na janga hili la Taifa. Mrisho Mpoto anakuwa Balozi mpya katika Kampeni hii kwa sababu ni msanii mwenye ushawishi ndani ya jamii na kupitia kazi zake za kisanaa tunaamini ataweza kuihamasisha jamii ipasavyo kuona umuhimu wa kumaliza tatizo la VVU na UKIMWI hasa katika masuala ya unyanyapaa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt. Fatma Mrisho, “Inakadiriwa kuwa watu milioni 1.6 nchini wanaishi na VVU & Ukimwi. Ugonjwa huo umewaathiri zaidi vijana na watoto yatima zaidi ya milioni 1.3. Tunahitaji kubadilisha hali hii.  TACAIDS kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na wadau wengine kwa kupitia mpango huu wa Kilimanjaro Challenge tunapenda kutoa mchango na ushirikiano wetu kwa Taifa ili kutunisha mfuko utakaowezesha kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo”.

Napenda kuupongeza  Mgodi wa Dhahabu wa Geita kwa kushirikiana na wadau wengine kwa kuamua kwa dhati kwa kipindi cha miaka 15 kuwekeza katika mradi huu kwa kuuwezesha kuwa mradi wa kitaifa na si wa GGM, hivyo pamoja na balozi wetu hivi sasa Mrisho Mpoto,  tuungane nao ili kuongeza chachu kwa wadau wengine kujitokeza kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya janga hili” alisisitiza Dkt Fatma Mrisho.

“Kwa kushirikiana na Mpoto tuna matumaini ya kujenga timu imara yenye hamasa ya kupambana na janga hili. Tunatoa wito kwa makampuni na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, wajitokeza ili tushirikiane kutunisha mfuko wa Kilimanjaro Challenge na mwishowe kufikia ndoto au malengo ya nchi yetu ya kuhakikisha tunakuwa na kizazi kisicho na maambukizi ya VVU na Ukimwi” alisema Bw. Simon Shayo Makamu wa Raisi wa miradi endelevu wa Anglogold Ashanti (GGM).

Shayo alisisitiza kwa kusema “GGM iko tayari kushirikiana na wadau wengine wenye nia ya dhati, kuungana pamoja kupitia mfuko wa Kili Challenge katika kuhakikisha maambukizi haya hayaendelei kuleta athari kwa jamii yetu kwa sababu serikali yenyewe haitaweza kutokomeza tatizo hili”.

Naye Balozi mpya wa Kili challenge, Mrisho Mpoto alisema; “Nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuweza kutoa mchango wangu katika kuisaidia jamii kuepukana na janga hili. Changamoto kubwa inayotokana na janga hili la VVU &UKIMWI ni ongezeko la maambukizi ya VVU kwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa letu pasipo kila mmoja wetu kujitoa kwa dhati hatutalimaliza janga hili. Napenda kuwaambia watanzania wenzangu kwamba tushirikiane kwa pamoja ili tuangamize janga hili”

Pamoja na hatua kubwa zilizopigwa na serikali ikishirikiana na wadau, kumekuwapo na ongezeko la maelfu ya watoto yatima wanaohitaji misaada baada ya wazazi wao kufariki, wajane wasiokuwa na kipato, pamoja na wazee wanaolazimika kuwalea wajukuu walioachwa na watoto wao ambao walifariki kutokana kwa ugonjwa huo alisisitiza Mkurugenzi mtendaji wa TACAIDS.

Kilimanjaro Challenge ni mradi unaolenga kutoa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa wa Ukimwi na Virusi Vya Ukimwi (VVU). Pia inalenga kuchangisha fedha ili kujenga timu imara itakayoendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo.Ili kuweza kuwa sehemu yawatakaopanda Mlima Kilimanjaro, kwa kupitia Kili Challenge mwaka huu, uwe Mtu binafsi au kupitia shirika kulipia wafanyakazi wake kupanda mlima mchango ni $5,000 tu ambazo zitalipia gharama za upandaji na kuchangia mfuko wa Kili Challenge.

Kilimanjaro Challenge imebakia kuwa chombo muhimu kinachoshirikiana na taasisi za nje na ndani ya nchi katika mapambano dhidi ya VVU&Ukimwi kwa jamii ya Kitanzania na dunia kwa ujumla ili kuwapa matumaini ya kuhakikisha jamii inabaki bila kuathiriwa na ugonjwa huo katika miaka ijayo
Mpango huo pia unalenga kuisaidia Serikali kukabiliana na VVU & Ukimwi pamoja  na kutoa nafasi kwa watalii wa ndani kuupanda mlima Kilimanjaro.


KUHUSU Kili Challenge:
Kwa maelezo zaidi tembelea tovuti ya www.anglogoldashanti.com  na www.geitakilichallenge.com

No comments: