Friday, May 20, 2016

DOLA ZA KIMAREKANI BILIONI 3 KUTUMIKA KUANZISHA MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA


Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage (kushoto) akiongea na Waandishi wa Habari (hawako pichani) kuhusu kuanza kwa mradi wa Mgodi wa kuchimba chuma na makaa ya mawe Liganga na Mchuchuma leo mjini Dodoma 19 Mei, 2016. Katikati ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayosimamia viwanda, biashara na uwekezaji, Mhe. Dkt. Dalaly Kafumu pamoja na Mkurugenzi Mwendeshaji toka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Bwana Mlingi Mkucha.



Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayosimamia viwanda, biashara na uwekezaji, Mhe. Dkt. Dalaly Kafumu (kulia) akisisitiza jambo mbele ya Waandishi wa Habari (hawako pichani) kuhusu kuanza kwa mradi wa Mgodi wa kuchimba chuma na makaa ya mawe Liganga na Mchuchuma leo mjini Dodoma 19 Mei, 2016. Kushoto ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage.



Baadhi ya Waandishi wa Habari waliohudhuria mkutano huo wakifuatilia taarifa toka kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage leo mjini Dodoma.
(Habari na picha na Benedict Liwenga, 
MAELEZO, Dodoma)

JUMLA ya dola Bilioni 3 za Kimarekani zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa  Mgodi wa Makaa ya  Mawe na Chuma wa Liganga na Mchuchuma.

Kauli hiyo imetolewa Leo mini Dodoma na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage wakati akiongea na Waandishi wa habari mini Dodoma.

Amesema mradi huo unaojengwa kwa ubia kati ya Tanzania Kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya China ya Sichuan Hongda Group unatarajia kuanza mwaka huu.

Mhe. Mwijage amesema kuwa fedha za kuwalipa fidia wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi huo ziko tayari ambapo zinatarajiwa kutumika zaidi ya bilioni 13 kwa ajili ya fidia na makazi.



Alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasadia kuzalisha umeme Megawati 600 ambapo 250 zitatumika katika Kiwanda cha Chuma na nyingine 350 zitapelekwa kwenye Gridi ya Taifa kwa ajili ya kuongeza nguvu katika nishati ya umeme.

‘’Pamoja na kuchimba chuma, Mradi wa Mchuchuma na Liganga utahusisha ujenzi wa Kinu cha Umeme chenye uwezo wa Megawati 600”, alisema Mhe. Mwijage.

Ameongeza kuwa, Tanzania kwa sasa itakuwa na umeme wa gesi, maji na umeme wa makaa ya mawe ambapo umeme wa makaa ya mawe utakuwa msaada mkubwa kwa nchi kwani hautegemei tabianchi kama ilivyo vyanzo vingine vya umeme.

Mhe. Mwijage amesema kuwa katika mradi huo, Tanzania itakuwa na hisa asilimia 20 na Mwekezaji kutoka China atakuwa na asilimia 80, lakini hisa za Tanzania zinaweza kuongezeka hadi kufikia 45. 

Chini ya mradi huo, Mwekezaji huyo anatakiwa kutoa elimu kwa Vijana katika ngazi zote za teknolojia zitakazohusika kutengeneza mgodi huo.

‘’Tutafundisha vijana wetu kwa ngazi tofauti kwani kampuni hii ni ya ubia kati ya Tanzania na China, tuna mamlaka sawa, tuna Wakurugenzi wetu wa Tanzania ndani ya hiyo kampuni, kwahiyo tutashiriki na hatutakuwa watazamaji”, alisema Mhe. Mwijage.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayosimamia Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambaye pia ni Mtaalam katika masuala ya madini, Mhe. Dkt. Dalaly Kafumu amesema kuwa, lengo la kuwajengea makazi wakazi wa maeneo ya mradi huo ni kuwawezesha wakazi hao kuwa na uhusiano mzuri na mgodi unaotarajiwa kujengwa.

‘’Serikali imeamua kuwajengea makazi wananchi ambao wanazunguka mradi Ili kuepusha wakazi hao kutumia pesa watakayolipwa kama fidia kwa matumizi mengine na kukosa makazi baadaye kuja kuilaumu Serikali kwamba imewadhulumu kwa kutowapa pesa za kutosha za kujenga nyumba”, alisema Dkt. Kafumu.

No comments: