Wednesday, April 13, 2016

WAGOMBEA NASAFI YA KATIBU MKUU UMOJA WA MATAIFA WAANZA KUHOJIWA

  Mgombea wa Nafasi ya  Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa, Bw. Igor Luksic ( Montenegro), akimwaga sera zake mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  wakati wa majadiliano/mhadalo  usio rasmi ulioandaliwa na  Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa lengo  kutoa fursa kwa wanaowania nafasi ya  Katibu mkuu kueleza sera zao na kisha kuulizwa maswali  
 Bi. Irina Bokova ( Burgalia) mmoja wa wanawake wanne waliojitokeza hadi sasa  kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa naye akijieleza mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. 
Bw. Antonio Guterres ( Portugal) mmoja wa wagombea waliohojiwa  katika siku ya kwanza ya mdahalo  usio rasmi wa kuwasikiliza wagombea waliojitokeza kuwaania nafasi itakayoachwa wazi na Ban Ki Moon, mwishoni mwa mwaka  huu. jumla ya wagombe tisa wamekwisha jitokeza mpaka jana ( jumanne).
  Taswira ya  Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa,  katika siku ya kwanza ya mdahalo wa kihistoria ya wagombea  nafasi ya  Ukatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mdahalo/majadiliano ya kwanza ya aina yake kufanyika katika   nafasi ya kumtafuta Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa .


Na Mwandishi Maalum, New York
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  jana ( Jumanne) limeandika historia kwa mara nyingine, kwa kuanza   mchakato usio  rasmi wa  kuwasikiliza na kuwauliza maswali  wagombea  watarajiwa waliojitokeza kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Mchakato huo ulianza kwa kuwasikiliza wagombea watatu kati ya tisa wakiwamo wanawake wake wanne  ambao hadi siku ya jumanne walikuwa wametangazwa rasmi kuwania nafasi hiyo itakayo achwa wazi na Katibu Mkuu wa  sasa   Ban Ki Moon anayemaliza muda  wake mwishoni mwa mwaka huu.

Katika awamu ya hiyo ya kwanza, kila  mgombea mtarajiwa  alipewa fursa ya kujieleza na kuelezea visheni yake,  sera, mipango, vipaumbele vyake  na nini anatarajia kukifanya  endapo  atachaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa  , Umoja  wenye wanachama 193.
Walioshiriki mdahalo huo katika siku ya kwanza  walikuwa ni  Dr. Igor Luksic ( Motenegro), Bi. Irina Bokova ( Bulgaria) na  Bw. Antonio Guterres ( Portugal)

Wengine ambao wamejitokea kuwania nafasi hiyo ni  Dr. Damilo Turk ( Slovenia) Prof.Dr. Vesna Pusic ( Crotia), Bi. Natalia Gherman ( Moldova), Dr. Srgian Kerim ( Macedonia),  Bi. Helen Clark ( New Zeland) na   Bw. Vuk Jeremic ( Serbia)

Ulikuwa ni mdahalo wa aina yake wa kwanza kutokea tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa miaka karibu  70  iliyopita, mdahalo  ulioendedeshwa katika  mazingira ya uwazi, na ambao kwayo umebadilisha kabisa utaratibu wa kumpata Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

 Mdahalo huo ambao  umeratibiwa na kusimamiwa na  Rais wa Baraza Kuu la 70 la Umoja wa Mataifa Bw. Monges Lykketoft, umetokana na makubaliano ya  pamoja kati ya  Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, na Rais wa Baraza la Usalama wakati huo ( mwezi  desemba) Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani. Na pia azimio  namba 69/321 la Baraza  Kuu la  Umoja wa Mataifa.

Katika  barua yao kwa wawakilishi wa kudumu wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa,  Bw.  Lykketoft na Balozi Samantha Power ( USA) walieleza juu ya kuwapo kwa  majadiliano au mdahalo wa wazi  na usio  rasmi  lakini muhimu   ambapo    makundi yote  yanayowakilisha nchi wanachama wa UN  yatapata fursa  ya kuwauliza maswali wagombea, maswali ambayo yamejielekeza  zaidi kwa maslahi ya makundi hayo, vipa umbele vyao na namna wanavyouona  Umoja wa Mataifa katika sura yake ya sasa.

Kama ilivyoelezwa hapo awali, hii ni mara ya kwanza kwa historia ya  Umoja wa Mataifa,   kwanza, kutoa fursa kwa wagombea wengi kujitokeza kuwania nafasi hiyo na kupewa nafasi ya kujieleza,  pili  nchi wanachama  wa Umoja wa Mataifa kupewa fursa ya kuwafahamu, kuwasikiliza na kisha kuwauliza na  maswali, na tatu  Asasi zisizo za kiserikali nazo kushirikishwa  katika mchakao huu. 

Vile vile ni historia ya   aina yake ambapo   kipaumbele kimetolewa kwa wagombea wanawake nao kujitokeza kuwania  nafasi hiyo ya juu kabisa katika Umoja wa Mataifa. Kwa takribani  mwaka mmoja sasa kumekuwapo  na kundi maalum ambalo lenye limejipambanua kama  marafiki wa mgombea mwanamke 

Mfumo wa uulizwaji wa maswali kwa wagombea hao ulikuwa ni ule  ambao Wenyeviti wa Makundi ya  Nchi wa wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Nne  (April ) ndio waliouliza maswali kwa  niaba ya makundi hayo. Aidha  hata  zile nchi ambazo  ni za visiwa au ambazo kwa lugha nyepezi  zimezungukwa na  mataifa  mengine (  land Locked countries) nazo zilipata  fursa ya kuuliza maswali yenye maslahi kwa  nchi zao.Kwa mfano  maswali ya  nchi za Afrika yaliulizwa na  Mwakilishi wa  Kudumu wa Uganda ambaye ni   Mwenyekiti wa Kundi la Nchi za Afrika kwa mwezi huu wa Nne.

Maswali  mengi waliyoulizwa wagombea,  yamejikita katika maeneo  mtambuka  kama vile  haki za binadamu,   operesheni za ulinzi wa Amani na utafutaji  suluhu  na  ufumbuzi wa migogoro, unyanyasaji wa kijisia unaofanywa na walinda Amani,   kuimbuka kwa  tatizo la ugaidi,  tatizo la wakimbizi, utekelezaji wa  malengo ya  maendeleo endelevu ( Agenda 2030), nafasi za  uteuzi kwa kuzingatia uwiano wa kijiografia na kikanda  katika ngazi za juu  za watendaji  katika sekretarieti ya Umoja wa Mataifa.

Maswali mengine yalihusu umalizwaji wa ukoloni,  utegemezi kwa wafadhili wachache katika uendeshaji wa Umoja wa Mataifa,  marekebisho ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yakiwamo kuongezwa kwa idadi ya  wajumbe wa kudumu wa baraza hilo,  weledi na sifa za uongozi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  na nini kifanyike ili kuufanya  Umoja wa Mataifa  kutekeleza  majukumu  yake ipasavyo kwa kuzingatia   mazingira   na hali  ya sasa na hususani kile kinachoelezwa kupoteza  mweleko wa  chombo  hicho  kikiuu cha kimataifa. 

Utaratibu uliozoeleka wa uchaguzi au uteuzi wa  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  ulibebwa zaidi na matakwa ya  Baraza  la Usalama na hasa kundi la   P5 ambao ni wajumbe wa kudumu wa Baraza hilo katika kupitisha  jina la waliyemtaka kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Baada ya Baraza   la Usalama, kupitisha jina la mteule waliyemtaka  jina hilo baadaye lilipelekwa  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambalo lilipitisha na halikuwa na uwezo wa kulikataa kwa kuwa limeshapitishwa na  Baraza la Usalama.

Utaratibu huu  umekuwa ukilalamikiwa na  Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa lenye wajumbe  193 kwamba  lilikuwa likitumikia kutia muhuli jina  ambalo limependekewa na wajumbe wachache ( Baraza la Usalama lenye wajumbe  15 wakiwamo watano wa kudumu).

Ni kwa sababu hiyo safari hii  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeamua kuchukua hatamu  na baada ya majadiliano ya kina baina ya nchi wanachama kuhakikisha kwamba  Baraza  hilo linakuwa na kauli au fursa    katika uteuzi wa Katibu Mkuu  badala ya kuwa watiaji  muhuri ( rubber stamp).

Leo  (jumatano) itakuwa ni zamu ya  Dr. Danilo Turk,   Prof.Dr. Vesna Pusic na Bi. Natalia Gherman. 

No comments: