Friday, April 8, 2016

TUNAWEZA KUIMALIZA MALARIA - JK

 Mhe Kikwete akiwa na ujumbe wake kutoka  kushoto ni Bw. Togolan Mavula,  Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi na Professa Mohamed Janabi
  Mhe. Kikwete akiwa na  sehemu ya wageni wakipata picha
  Mhe Rais Mstaafu akiwa na Bw. Ray Chambers na Mkewe Bi. Patti Chambers muda  mfupi kabla ya  hafla ya kuanza.
  Mhe Kikwete akiwa na  Bw Blitzer mtangazaji maarufu wa CNN kupitia kipindi chake cha  Situation Room
 Mwanzilishi wa  Malaria no More, Bw Peter Chernin akimkabidhi Mhe. Rais Mstaafu, Kikwete  tuzo ya White House Summit Awards ikiwa ni kutambua na kuthamin mchango na uongozi wake katika jitihada za kuukabili  ugonjwa wa malaria, wengine waliopewa tuzo hiyo ni Bw. Ray Chambers na Kampuni ya  Sumitomo Chemical  ambayo imejenga kiwanda cha vyandarua cha A-Z Arusha Tanzania.
  Rais Mstaafu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akielezea  juhudi zilizofanywa na  serikali ya Tanzania katika kuukabili ugonjwa wa malaria, ilikuwa wakati wa hafla ya miaka 10 ya Malaria no More iliyofayika jana alhamis New York Marekani, Mhe. Kikwete amealikwa katika hafla hiyo   kutokana na mchango wake mkubwa katika pamoja na  mengin kuwahamasisha viongozi wa Afrika kuongeza juhudi za kisera, kimkakati na bajeti  hali ambayo imechangia sana katika  kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano. pamoja naye ni  Bw. Peter Chernin, Bw. Ray Chambers na mwezeshaji,  Bw. Wolft Blitzer wa CNN.
  Sehemu  ya Wageni zaidi ya 250 kutoka masharika na makampuni mbalimbali  ambako ni sehemu ya wadau wa kubwa wanaochangia juhudi za kutokomeza na kudhibiti ugonjwa wa malaria.
  Mhe. Rais Mstaafu katika mkutano na Bodi mpya ya Malaria no More muda mfupi kabla ya kuanza kwa hafla ya miaka 10 ya Malaria No More
Burudani pia ilikuwapo.


 
Na Mwandishi Maalum, New York

Rais Mstaafu wa awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amesema, anaimani kubwa kwamba  ushirikiano  uliopo  baina ya serikali mbalimbali barani Afrika,  mashirika ya kimataifa, makampuni binafsi  na kila mtu katika nafasi yake, hapana shaka ugonjwa wa malaria unaweza  kumalizwa kabisa.

Mhe. Kikwete ameonyesha matumaini hayo   jana( alhamisi) wakati wa hafla  ya kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa jitihada za  kuutokomeza   ugonjwa wa malaria ( Malaria No More) zilizoanzishwa na  Bw. Ray Chambers akishirikiana na  Bw. Peter Chernin.

Katika  hafla hiyo na ambayo  mshereheshaji alikuwa Bw. Wolf Blitzer mtangazaji maarufu wa Televisheni ya Kimataifa  ya CNN kupitia kipindi chake cha situation Room, Rais  mstaafu alitunukiwa tuzo ijulikanayo  kama  White House Summit Awards ikiwa ni kutambua uongozi wake,   kujitoa kwake na  kubwa zaidi kusimamia  uanzishwaji wa muungano wa viongozi wa Afrika dhidi ya Malaria ( ALMA) muungano ambao   hadi sasa una viongozi 49.Wengine waliotunukiwa tuzo hiyo ni  Bw. Ray Chambers na Sumitomo Chemical.

Akijibu swali la nini anadhani kumechangia katika kupunguza idadi  ya  vifo vitokanavyo  na   ugonjwa wa malaria. Rais  mstaafu  amesema, zipo sababu kadhaa, lakini  kubwa ni  utashi wa kisiasa wa kusimamia na kuongoza mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Akawaeleza wageni zaidi ya 250 walioalikwa wakiwa ni wawakilishi wa makapuni na mashirika mbalimbali  yanayochongia juhudi za kuukabili ugonjwa wa malaria. Kwamba, Upatikanaji  na usambazani wa dawa sahihi za kutibu ugonjwa wa  malaria,  utengenezaji,  usambazaji na matumizi ya vyandarua vyenye viatilifu na unyunyiziaji wa dawa za kuuwa mazalia ya mbu ni mambo ya msingi ambayo  yamechangia katika  kupunguza  vifi vya watoto chini ya miaka mitano.

“mchanganyiko wa mambo hayo matatu umesaidia sana kupunguza idadi ya  watoto wanaofariki kwa malaria, lakini pia matumizi ya  vyandarua vyenye viatilifu ambapo zaidi ya vyandarua  milioni 24.2 vimesambazwa,  kumechangia wanafunzi kuendelea na masomo yao bila kukatishwa mara kwa mara sababu ya malaria, halikadhalia nguvu kazi imeimarika”. akasisitiza Rais Kikwete na kushangiliwa na  wageni waalikwa.

Akaongeza kwamba ugonjwa wa malaria unatakiwa kutokomezwa Barani Afrika kwa sababu unapoteza maisha ya watu wengi, bajeti kubwa katika huduma ya afya inatumika katika kutibu  ugonjwa wa malaria, lakini  uchumi unaathirika kutoka na nguvu kazi kuugua mara kwa mara.

Akasisitiza  “ Malaria inaweza kutokomezwa. Zanzibar wameweza kutokemeza malaria,  mkienda Zanzibar kutembea msiwe na wasi wasi kupata malaria”. akasema na kushangiliwa tena na wageni.

kwa  upande wake,  Mwanzilishi wa  Malaria No More Bw. Ray Chamber, pamoja na kuelezea historia fupi ya   Malaria no more ilikoanzia na ilipofika na nini mipango ya baadaye. Amemuelezea Rais  Mstaafu  Kikwete kama kiongozi ambaye siyo tu amekuwa mstari wa mbele katika kuukabili ugonjwa wa malaria  bali pia amekuwa kiungo muhimu sana katika  mapambano hayo.

“Wakati nimeanzisha juhudi hizi, nikawa natafuta  mahali pakuwa   na center moja na hasa kwa kuzingatia kwamba Afrika  kuna nchi 43 ambazo  zinatatizo kubwa la malaria, nilikuwa Benin na Mke wangu  tukawa tunajadili pa kuanzia. Nikampigia simu Rais Kikwete na kumweleza nini nilichokuwa nataka kufanya. Akanijibu  haya na tufanye. Sijawahi kuwa na rafiki kama  Rais Kikwete na kwa ushirikiano wake tumefika hapa” akasema Bw. Chambers na kushangiliwa.

 Akabinisha kwa kusema. “Kikwete amekuwa kiongozi wa kwanza kufanya  kazi nami  ,  kushirikiano  wake  alionipa, ushirikiano  na wabia mbalimbali  mkiwamo nyingi hapa  katika ukumbi huu,  Marais wa Marekani,  Banki ya Dunia,  Global Fund, Bill and Melinda Gates Foundation, tumeweza kupunguza vifo vitokanavyo na malaria kwa asilimia 71 na tumeokoa maisha ya watu wengi.

Bw Ray Chambers ambaye pia ni mjumbe  maalum wa  Katibu Mkuu wa Umoja  wa Mataifa kuhusu Malaria, anasema katika miaka  kumi ya  uhai wa Malaria no More lengo na mikakati waliyonayo sasa  ni kutokomeza  kabisa malaria ifikapo 2040.

Kwa upande wake, Mwanzilishi mwenza na Mwenyekiti wa Malaria no More Bw. Peter Chernin,  amesema,  katika kuonyesha ni  namna gani Rais  Mstaafu Kikwete amekuwa mstari wa mbele dhidi ya ugonjwa wa malaria, alianzisha   na Mama Salma  kampeni ya “zinduka Malaria haikubaliki” kwa lengo la  kuwahamasisha wananchi na kutoa elimu  dhidi ya malaria juhudi ambazo zinazaa matunda.

Akaongeza kwamba,utashi wa kisiasa upo,  utayari upo, sayansi  ipo,  nyenzo  zipo, kinachotakiwa  ni fedha tu. Na kwa sababu hiyo akatoa  wito kwa  wadau wote  wenye mapenzi mema kuchangia chochote walichonacho ili  juhudi za  kuokoa maisha ya watu wenzi zaidi wakiwamo watoto iendelee ikiwa ni  pamoja na   kuitokomeza malaria katika uso wa dunia.

Naye mwakilishi wa Kampuni ya  Sumitomo Chemical, Bw. Ray Nishimoto  pamoja na kuelezea  kazi kubwa iliyofanywa na kampuni ya A-Z katika kutengeneza vyandarua vyenye  viatilifu amesema bila juhudi na ushirikiano wa karibu aliouonyesha Rais Jakaya Kikwete  kiwanda hicho kisingejengwa Arusha- Tanzania.

Akasema licha ya kutoa mchango mkubwa katika  kuudhibiti ugonjwa wa malaria Kiwanda cha A-Z kimetoa ajira kwa watu 8,000 asilimia kubwa wakiwa ni wanawake na kwamba  Sumitomo Chemical itaendelea na jitihada hizo.

No comments: