Wednesday, April 27, 2016

Siku ya Uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Na Eleuteri Mangi-MAELEZO.

Wanadamu wameumbwa kwa hulka na silika ya kuwa na uwezo wa kuwasiliana miongoni mwao, jamii wanamoishi, taifa na hata ulimwenguni ili waweze kutimiza nia na azma yao ya kuwasiliana.Ili mawasiliano hayo yakamilike ni lazima yabebe ujumbe unaokusudiwa kufikishwa katika jamii.

 Ujumbe huo ili uweze kumfikia mlengwa, ni lazima iwepo njia ya kuufikisha ujumbe huo kwa mlengwa ambao huwasilishwa kwa maandishi (magazeti), sauti (redio) na picha (TV) pamoja na mitandao ya kijamii kupitia huduma ya inteneti.Vyombo hivyo vya habari vinahusisha wataalamu ambao kazi yao ni kuhakikisha jamii inapata ujumbe kwa wakati ili kuweza kujenga, kuboresha na kuimarisha maisha yao kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.

Vyombo vya habari hakika vimekuwa ndio macho na masikio ya wananchi ili kufikisha ujumbe unaohusu mambo mbalimbali yanayofanyika ndani na nje ya nchi.
Tunapoelekea siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Mei 2 na 3, maadhimisho hayo mwaka huu yataadhimishwa nchini Finland, ambapo wanahabari wote duniani wataungana kuwakumbuka wenzao waliofariki dunia walipokuwa wakitekeleza majukumu yao na kupanga mipango mipya ya namna watakavyoboresha kazi zao ziwe za ufanisi zaidi.
Tanzania ikiwa miongoni mwa mataifa ya dunia hii, nayo haipo nyuma katika suala la uwepo wa vyombo vya habari.

Ni dhahiri vyombo vya habari nchini vimekuwa kiungo muhimu katika kisaidia Serikali kutoa taarifa mbalimbali na ajira hatua ambayo imesaidia kupunguza tatizo la ajira nchini.Ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki, Tanzania inayoongoza kwa kuwa na vyombo vingi vya habari, hali ambayo ni msingi wa kuajiri watu wengi zaidi katika tasnia hiyo.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye ambaye ndiye mwenye dhamana ya habari nchini anasema Serikali inaunga mkono juhudi zinazofanywa na vyombo vya habari nchini.“Tulipofika ni pazuri ukilinganisha na tulipotoka, mengi yamefanyika hasa ukiangalia idadi ya vyombo vya habari nchini na uhuru wa waandishi wa habari wanavyoanadika na wanavyofikisha ujumbe kwa wasomaji, wasikilizaji na watazamaji” alisema Waziri Nape.

Aidha, Waziri Nape amesema kuwa bado Serikali inakusudia kuboresha mazingira ya waandishi wa habari ili waweze kufanya kazi zao kwa hali ya uhuru hasa wanapotimiza majukumu yao ya kiundishi wa habari.Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambacho ni chombo kilichoanzishwa kisheria kusimamia sekta za mawasiliano na utangazaji nchini hadi sasa kuna jumla ya vituo kadhaa vya radio na televisheni vilivyosajiliwa.

Idadi ya vituo vya redio vilivyosajiliwa nchini hadi sasa ni 123 ambavyo ni sawa na asilimia 43.4 katika ukanda wa Afrika Mashariki huku miongoni mwa vituo hivyo vinamilikiwa na makampuni binafsi, taasisi na mashirirka ya dini, jamii na Serikali ambayo inayomiliki kituo kimoja cha TBC Taifa inayoendeshwa chini ya Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC), nchini Kenya vipo vituo vya redio 118 sawa na asilimia 41.7, Uganda 37 sawa na asilimia 13.1, Rwanda vituo vitatu sawa na asilimia 1.1 wakati Burundi ina vituo vya redio viwili ambavyo ni sawa na asilimia 0.7.

Kwa upande wa vituo vya televisheni, Uganda inaongoza kwa kuwa na vituo vingi ambavyo idadi yake ni 44 sawa na asilimia 53.6, ikifuatiwa na Tanzania yenye vituo 24 sawa na asilimia 29.3, Kenya vituo 10 sawa na asilimia 12.2, Rwanda vituo vitatu ambavyo ni sawa na asilimia 3.7 na Burundi ikiwa na kituo kimoja cha televisheni ambacho ni sawa na asilimia 1.2 

Kwa kuzingatia maslahi ya wananchi na wamiliki wa vyombo vya habari na wanahabari wenyewe, TCRA imekuwa ikihimiza juu ya ufanisi wa ushindani na uchumi, kulinda maslahi ya walaji, kulinda uwezo wa fedha na ufanisi wa wagavi.

Pia inahimiza upatikanaji wa huduma zinazosimamiwa kisheria kwa walaji wakiwemo wenye kipato cha chini na walaji wa vijijini na wa pembezoni, kukuza mwamko, maarifa na uelewa wa jamii kuhusu sekta zinazosimamiwa ikiwemo kuzingatia haja ya kulinda na kuhifadhi mazingira, haki na wajibu wa walaji na wagavi wanaosimamiwa.

Katika kuonesha Tanzania inavyosimamia uhuru wa vyombo vya habari, TCRA ina jukumu lingine la kusimamia malalamiko na migogoro inayoweza kujitokeza miongoni mwa wateja wake wakiwemo wamiliki wa vyombo vya habari, wananchi na kupatia ufumbuzi changamoto hizo. 

Aidha, hadi Aprili 22, 2016, Tanzania imekuwa ndio nchi inayoongoza Afrika Mashariki kwa kuwa na idadi kubwa ya magazeti yaliyosajiliwa ambapo idadi yake ni 881 licha ya magazeti na majarida mengi kusajiliwa, mengi huchapishwa mara chache na mengine kutokuchapishwa na kusambazwa baada ya kusajiliwa.

Kwa idadi ya magazeti nchi za Uganda, Rwanda na Burundi yapo magazeti matano yanayotumika katika nchi hizo wakati Kenya ina magazeti saba ambayo husomwa na kufikisha ujumbe kwa walengwa katika mataifa hayo.

Wingi huo wa vyombo vya habari nchini imekuwa ishara njema ya kujali uhuru wa kuanzishwa kwa vyombo vya habari kwa makampuni binafsi, taasisi na mashirika ya dini pamoja na jamii mbalimbali ili kuweza kuwa ndio namna yao ya kupata taarifa.  
Katika ulimwengu wa leo, uhuru wa habari ni suala la msingi na lina umuhimu mkubwa katika kutekeleza haki za binadamu katika kutafuta, kupata, kupokea na kutoa habari ambazo ni muhimu kwa nchi katika kujiletea maendeleo endelevu.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inawahimiza wanahabari na watu wote kutambua “Kupata Habari ni Uhuru wa Kimsingi: Hii ni haki yako!” ikilinganishwa na kauli mbiu ya mwaka uliyopita ambayo ilisema “Achia uwandishi habari ustawi! Kuelekea upashaji habari bora, usawa wa jinsia na usalama wa vyombo vya habari katika enzi ya dijitali”.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Aprili 8, 2016 imebainisha kuwa katika maadhimisho ya Siku ya vyombo vya habari duniani mwaka huu, mwandishi wa habari za uchunguzi kutoka Azerbaijan Khadija Ismayilova amechaguliwa kupokea tuzo ya uandishi wa habari za uchunguzi ijulikanayo “Guillermo Cano” inayotolewa na Shirika hilo.

Tuzo hiyo ina thamani ya Dola za Kimarekani 25,000, na imepoewa jina hilo kwa heshima ya Guillermo Cano Isaza, mwandishi wa habari wa Colombia aliyefariki Desemba 17, 1986 akiwa kazini.Jukumu la kuenzi na kutoa tuzo ya heshima kwa waandishi wa habari duniani linafadhiliwa na taasisi ya Cano Foundation kutoka nchini Colombia na Helsingin Sanomat Foundation kutoka nchini Finland.

Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano na Habari UNESCO Frank La Rue anasema "Uhuru wa vyombo vya habari ni muhimu kwa taarifa muhimu na uwazi ni ambao ni mahitaji ya jamii ya kidemokrasia. Lakini leo tunaona ongezeko la ghasia na vitisho dhidi ya waandishi ambayo mimi napendekeza nchi zote duniani kuanzisha utaratibu wa habari na ulinzi kwa ajili ya usalama wa waandishi wa habari"
Moja ya changamoto za kuweka utaratibu wa usalama wa waandishi wa habari ni idadi ndogo ya mifano ya taratibu zilizopo ambayo inaweza kuwa somo ili wengine waweze kujifunza kutokana na taratibu zilizopo. 

Masuala muhimu ya kuzingatiwa wakati wa kuanzisha utaratibu huo ni pamoja na kuwepo kwa makundi matatu ambayo ni wigo wa utaratibu, ushirikishwaji wa wadau muhimu pamoja na taasisi kubuni  na kutathmini hatua ambayo itasaidia kufikia malengo ya kumlinda mwandishi wa habari.

Akizungumzia maandalizi ya maadhimisho kitaifa ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari nchini ambayo yanafanikia jijini Mwanza Mei 2 na 3, mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho hayo Andrew Marawiti amesema kuwa yanaendelea vizuri kulingana na ratiba ilivyopangwa.

Katika maadhimisho hayo, Marawiti amesema kuwa Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Othman Chande ambapo wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo mada mbalimbali zitawasilishwa na watoaKuhusu ratiba ya siku mbili za maadhimisho hayo, Marawiti amesema kuwa zitawasilishwa zikiandamana na majadiliano kwa washiriki wote.

Miongoni mwa washiriki wanaotarajiwa kuwepo katika maadhimisho hayo ni wadau mbalimbali wa habari wakiwemo viongozi wa Serikali, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, wamiliki wa vyombo vya habari, waandishi wa habari na wananchi.

Kulingana na takwimu zilizopo, mwandishi wa habari mkongwe nchini, Mzee Willie Mbunga amesema kuwa Tanzania ina vyombo vingi vya habari ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo kulikuwa vyombo vichache vya habari ambavyo ni redio Tanzania Dar es salaam, Tanganyika Standard, Mambo Leo, Uhuru, Mzalendo na Ngurumo. 

Aidha, amesema kuwa changamoto ya baadhi ya watu kujisahau na kuweka pembeni maadili ya uandishi wa habari ni suala ambalo si la kufumbiwa macho, ni vema litiliwe maanani ili kukiokoa kizazi cha sasa na kijacho katika kujenga jamii inayojali na kusimamia maadili ya taaluma na ya jamii.

Katika upashanaji habari, dunia sasa imekuwa sawa na kijiji hasa katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia ambapo mawasiliano ndio imekuwa nguzo ya kila kitu.
Awali makala haya yameonesha kuwa ujumbe katika jamii ulifikishwa kwa njia ya redio, magazeti na TV, zaidi ya vyombo hivyo, mitandao ya kijamii kwa sasa imekuwa nguzo mahiri na vyanzo vikuu vya habari kwa waandishi wa habari na wananchi.
Miongoni mwa mitandao hiyo ya kijamii ni pamoja na blog ya Serikali, Michuzi, fullshangwe, bayana, milardayo, mwamba wa habari, businessmagnetblogs, mpekuzi, moh Dewji na mitandao mingine.

Mwandishi wa habari Majid Mjengwa ambaye pia ni mwanzilishi na mmiliki wa blog ya mjengwa anasema “Mitandao ya kijamii imekuwa ni eneo la upashanaji habari linalofanya kazi kama vyombo vingine vya habari”.

Ili kufikisha ujumbe kwa jamii, Mjengwa amesema kuwa watu wote wanaofanya kazi katika mitandao ya kijamii wanapaswa kufuata maadili ya taaluma ya habari pamoja na sheria na taratibu za nchi husika ili kuondoa mgongano wa maslahi katika kufikisha ujumbe kwa jamii.

Ni dhahiri haki na wajibu ni vitu ambavyo haviachani, hivyo ni jukumu la kila mdau wa habari nchini wakiwemo Serikali, waandishi wa habari, wamiliki wa vyombo vya habari na wananchi kuzingatia sheria, kanuni, taratibu pamoja na maadili ya jamii.
Hatua hiyo itasaidia kuimarisha na kuhakikisha wadau hao wanakuwa sehemu ya kujenga uhuru wa vyombo vya habari ambavyo vitakuwa chachu ya kujenga taifa imara lenye uchumi bora kwa manufaa ya Watanzania ifikapo mwaka 2025. 

No comments: