Thursday, April 28, 2016

Nape Apania Kuiboresha Tasnia ya Habari

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye akikabidhi Ipad tano kwa mkuu wa wilaya ya Bukoba Bw.Jackson Msome kwa ajili ya matumizi ya maafisa habari wa mkoa wa Kagera. Bwana Msome alikuwa akimwakilisha Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Mustafa kijuu.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Sekta ya habari ni kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya wananchi na serikali yao. Ndiyo maana wanazuoni hupenda kusema kuwa habari ni muhimili wa nne wa dola. Kwa kuzingatia umuhimu huo, katika kuchekecha huku na huko, Mhe. Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akamteua mtu mahiri kuongoza sekta hii, Mhe. Nape Moses Nnauye.

Kwa uteuzi huu ninadiriki kusema hatimaye Wizara imepata mtu sahihi na mchapakazi anayeweza kwenda na kasi ya Mheshimiwa Rais Magufuli na ni dhahiri kabisa kuwa kumpa Mhe. Nape ni kuthibitisha usemi wa wahenga usemao upele umepata mkunaji.

Kwa jinsi hii tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Nchi kwa kutujalia kupata kiongozi wa nchi ambaye ni mchapakazi na aliyejaliwa kipawa cha kuona mbali kwa kuwaweka viongozi wa chini yake katika nafasi za uongozi wanazostahili.

Sekta ya habari ni sekta nyeti na muhimu sana katika dunia hii kwa kua bila kupashana habari na kujua kinachoendelea daima hakutakua na maendeleo kwa hiyo, ni sekta inayohitaji kuangaliwa kwa jicho la tatu ili kuhakikisha kwamba inachukuliwa uzito na inapewa kipaumbele kwa kupewa vifaa na elimu ya kutosha ili kuepusha upotoshaji na kukosekana kwa habari muhimu hasa za Serikali zinazotakiwa kuwafikia wananchi kwa muda husika.

Tukiangalia katika sekta ya habari, Mhe.Rais hakukosea kabisa kumuweka Waziri Mhe. Nape kwa kuwa ameanza kuitumikia Wizara kwa kasi nzuri na ameonyesha nia ya kuiboresha Wizara hasa kwa tasnia ya habari kwa kuanzia kwenye wizara yake hadi katika ofisi za umma zilizoko mikoani ili kuhakikisha wanahabari wote nchini wanatambua thamani ya kazi yao. 

Kwa maneno yake aliyoyatoa Jijini Mbeya alipokua akigawa vitendea kazi vya kisasa kwa ajili ya mawasiliano yaani ipad kwa maafisa mawasiliano wa mkoa huo alikaririwa akisema,"Nataka Wizara ihamie mikoani" hii haimaanishi kuwa Wizara ihamie mikoani kama alivyosema bali alimaanisha kiutendaji zaidi kuwa yale yote anayoyafanya katika Wizara yake atahakikisha na maafisa wa mikoani pia wanafanyiwa hivyo ikiwemo kugawiwa vitendea kazi pamoja na mambo mengine. 

Katika kuhakikisha hilo, kwa upande wa sekta ya habari, Waziri Nape ameanza kwa kugawa ipad  kwa maafisa mawasiliano walioko mikoa ya pembezoni ambao wana upungufu mkubwa wa vitendea kazi na kwa muda mrefu wameshindwa kuifanya kazi yao kwa ufanisi kwa sababu ya uhaba wa vifaa vya kufanyia kazi hiyo.

Ipad hizo zilizotolewa kama msaada kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na kampuni ya Startimes ambayo imeahidi kuwa bega kwa bega na Wizara hii  katika kuisaidia ili kuongeza ufanisi hasa katika sekta hii nyeti ya habari maana kwa maneno mengine tunaweza kusema sekta ya habari ndio daraja linalounganisha serikali na wananchi.

Siku aliyokabidhiwa ipad hizo Mhe. Nape alikaririwa akisema "Nawashukuru sana Startimes kwa kutujali,ipad hizi tutaanza kuzigawa kwa maafisa habari wa mikoa ya pembezoni kwa kuwa ndiko kuna uhaba mkubwa sana wa vifaa kwa maafisa hao"alisema Mhe Nape.

Maneno haya ya Mhe.Nape yanaungana na usemi wake wa kuifanya Wizara kuhamia mikoani kwa maana ya kuwapa kipaumbele katika kuwapatia vitendea kazi ili nao wasijione kuwa wametengwa au kutokuthaminiwa kama maafisa mawasiliano wengine hasa walioko Dar es salaam na mikoa mingine iiliyoendelea. Maana anaamini kuwa mikoani ndiko kuna wadau na ndiko ziliko shughuli nyingi kwa kuwa watu wengi wenye uwezo wa kuzikuza tasnia anazozifuatilia wapo mikoani.

Ni mengi sana Mhe.Nape ameyaongea hasa kwenye ziara zake alizozifanya kwenye baadhi ya mikoa kama Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Geita, Simiyu,Dodoma, Kagera pamoja na Mwanza ambako alipita kugawa ipad na kuangalia jinsi maafisa habari wanavyofanya kazi katika vituo vyao vya  kazi. Ziara hiyo pia inalenga katika kujua changamoto wanazokumbana nazo ili kuweza kufanya kila kinachowezekana kuzitatua ili kufanya sekta hii kufanya kazi ya kupeleka taarifa kwa wananchi kama inavyopaswa kufanyika ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Jemedari Mkuu Mhe. Rais John Pombe Magufuli.

Kiongozi huyu ameongelea kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ambao ulishirikisha wadau mbali mbali hasa wahariri pamoja na wamiliki wa vyombo vya habari kutoa maoni yao ambayo kwa asilimia 99 maoni hayo yamewekwa katika muswada huo.

"Muswada huo umeshakamilika, uko tayari kufikishwa bungeni, pia nataka niwathibitishie kuwa muswada huo utalinda maslahi ya waandishi wa habari kuanzia mishahara yao, mikataba ya kazi zao pamoja na bima ya matatizo wanayoyapata kwenye kazi zao lakini muswada huo utakua na sheria zitakazobana ufundishwaji wa masomo ya habari ili tupate waandishi ambao wamebobea katika fani hiyo" alisema Mhe. Nape.

Ndoto ya changamoto zinazoikabili tasnia ya habari mikoani zinakaribia kuwa historia kwa kuwa Waziri Nape amepanga kuleta teknolojia mpya na kuzitoa zile zilizopitwa na wakati ili kuharakisha ufanisi wa utoaji wa taarifa, kuweka busta kwa baadhi ya maeneo ili televisheni ya taifa (TBC) iwe bora zaidi na kuongeza urefu wa minara ili matangazo yafike mbali zaidi.

Waziri Nape ameamua kuboresha urefu wa minara ili matangazo yafike mbali kwani mikoa mingi ya pembezoni imepakana na nchi ambazo teknolojia zao za mawasiliano ni kubwa kiasi kwamba wananchi wengi wa mipakani wanasikiliza redio za nchi jirani na kuacha kusikiliza redio za hapa nyumbani Tanzania.

Katika harakati za kuboresha tasnia ya habari, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos Makalla ameelezea changamoto na jinsi alivyopanga mikakati ya kusaidia na kuiboresha tasnia hii mkoani kwake ambapo alikaririwa akisema "Mkoa wangu unaomba kibali cha kuajiri maafisa habari ili kila Halmashauri iwe na afisa habari wake pia naahidi kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kununua vitendea kazi vya maafisa hao".

Wakati huo huo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa wito kwa wananchi kuanzisha vituo vya utangazaji 19 katika Wilaya na Halmashauri mbalimbali na wamewaomba wadau kutuma maombi kabla ya Aprili 29 mwaka huu.

Akiongea katika mkutano wa Mhe.Nape na wadau wake, Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Lilian Mwangoka alisema, "Mamlaka ya Mawasiliano ipo tayari kushirikiana na wananchi kuongeza vituo vya utangazaji ili kuongeza idadi ya vituo na kuongeza fursa katika ukusanyaji wa kodi".

Aidha, Waziri Nape amesisitiza suala la maafisa habari kupewa ruhusa ya kushiriki katika vikao vya maamuzi ili wajue mambo yanayoendelea katika ofisi zao kwani kufanya hivi kutasaidia maafisa habari kuacha kuwakimbia waandishi wa habari na badala yake kuwapa taarifa kamili ili wakawajulishe wananchi taarifa sahihi kuhusu Serikali yao.

Akiongea kwa kujiamini Waziri Nape amehakikisha kuwa yote yatawezekana maana fedha za kutatua kero hizo zitapatikana kwa kuwa Mhe.Rais tayari alifanya maamuzi ya kuziamuru taasisi zote za Serikali zilizopewa huduma ya kutoa matangazo yao kupitia Televisheni ya Taifa bila kulipa waanze kulipa madeni yao mara moja kwa hiyo fedha hizo ndizo hasa zitatumika katika kuboresha tasnia hii.

Sasa ni wakati wa maafisa habari pamoja na waandishi wa habari wote nchini kuunga mkono jitihada za waziri wetu kwa kufanya kazi za kukusanya na kutawanya taarifa kwa ufanisi na usahihi wa hali ya juu  ili kuifanya jamii ielewe umuhimu wetu pamoja na kukuza uchumi wa nchi kupitia taarifa tunazozitoa kwenye vyombo vya habari.

Wahenga wanasema Taifa lisilo na taarifa haliwezi kukua kiuchumi, litadumaa. Hivyo tumuunge mkono Mzalendo huyu ili kukuza na kuinua Tasnia ya Habari na ionekane kweli kuwa muhimili wanne wa dola ambao unachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta maendeleo.

No comments: