Friday, April 22, 2016

JAJI MKUU AWATAKA WATUMISHI WA MAHAKAMA MKOA WA MBEYA KUFANYA KAZI YA UTOAJI HAKI KWA UADILIFU.

JAJIMkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, amefanya ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua shughuli za Mahakama katika Kanda ya Mbeya. 
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman  akiweka sahihi katika kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Mahakama ya Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya.

Ziara ya Mhe. Jaji Mkuu katika kanda hii imelenga kujionea hali ya utendaji kazi wa Mahakama katika mkoa huo ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha Watumishi wa Mahakama kufanya kazi kwa ufanisi na weledi ili kuboresha huduma ya utoaji haki nchini. 

Katika ziara yake Mhe. Jaji Mkuu aliambatana na Maafisa na Watendaji kadhaa wa Mahakama kutoka Makao makuu ili kujionea hali ya utendaji kazi ikiwa ni pamoja na kubainisha na kufanyia kazi changamoto ambazo watumishi wanakumbana nazo katika utendaji kazi wa kila siku. 
 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, (katikati) akipata taarifa fupi ya utendaji kazi wa Mahakama Kanda ya Mbeya kutoka kwa Mhe. Noel. P. Chocha, Jaji Mfawidhi Kanda ya Mbeya (aliyesimama), mara baada ya kuwasili katika kikao kilichohusisha Mahakimu Wakazi Wafawidhi,Watendaji, Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala wa Kanda ya Mbeya.

Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye alipata nafasi ya kukagua na kuongea na Watumishi wa ngazi mbalimbali za Mahakama katika mkoa huo.

Katika kikao alichofanya na Watumishi wa Mahakama mkoani humo ikiwa ni pamoja na Wahe. Majaji na Mahakimu, Mhe. Jaji Mkuu alisisitiza mara zote juu ya utendaji kazi kwa kujituma ili kubadili taswira ya Mahakama kwa wananchi ambao ndio wadau muhimu wa Mahakama.
Akiongea na Watumishi wa Mahakama wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Jaji Mkuu alieleza kufurahishwa na kasi ya usikilizaji na umalizwaji wa mashauri katika Mahakama za Mwanzo mkoani humo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman akizungumza na  Mahakimu Wakazi Wafawidhi,Watendaji, Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala wa Kanda ya Mbeya alipokutana nao na kuwaasa kuendelea kutenda Haki kwa wakati ili kuweza kupunguza na kumaliza mashauri yanayowasilishwa mahakamani.

Awali; katika taarifa yake kwa Mhe. Jaji Mkuu, Mhe. Noel Chocha, Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, alimtaarifu Mhe. Jaji Mkuu juu ya mkakati waliojiwekea wa kumaliza mashauri ya aina yoyote kwa kipindi kisichozidi miezi sita. 

Aidha Mhe. Jaji Mkuu alitumia ziara hiyo ya kikazi kuwaeleza Watumishi juu ya mikakati ambayo Mahakama imejiwekea katika kuhakikisha kuwa huduma ya utoaji haki inaboreshwa nchini. 

“Kwa hivi sasa Mahakama ya Tanzania imejiwekea mikakati/vipaumbele ambavyo vinalenga kuboresha huduma ya utoaji haki nchini, na malengo haya inabidi yafanyiwe kazi na kila mmoja wetu kwa maana ya kila Mtumishi na mdau wa Mahakama awajibike katika kufikia malengo yetu ya kuboresha huduma ya utoaji haki nchini.” Alisema, Mhe. Jaji Mkuu.

Uimarishaji wa ukusanyaji wa takwimu; hili pia ni eneo ambalo limewekwa kama kipaumbele katika maboresho Mahakamani, Mhe. Jaji Mkuu alisema Mahakama pia imejipanga vyema kuhakikisha inakuwa na takwimu sahihi za kesi mbalimbali zilizopo katika Mahakama mbalimbali nchini ili kuangalia ni sehemu ipi inayohitaji nguvu zaidi katika kushughulikia mashauri/kesi za muda mrefu. 

Uboreshaji wa Miundombinu: miundombinu hii ni pamoja na majengo ya Mahakama, vitendea kazi n.k, Mhe. Jaji Mkuu alisema pia katika kuboresha huduma zake Mahakama imejipanga katika kuboresha miundombinu yake ikiwa ni pamoja na kujenga majengo ya Mahakama na kukarabati majengo yaliyochakaa. 

“Tatizo kubwa ambalo Mahakama inakabiliana nalo ni uchakavu wa miundombinu yake, kwa hili tuko mbioni kuhakikisha Mahakama inakuwa na miundombinu bora zaidi, tumejipanga kuboresha ikiwa ni pamoja na kujenga Mahakama Kuu katika mikoa yote ambao haina majengo, taratibu zinaendelea na kwa mwaka huu tumepanga kuanza ujenzi wa Mahakama Kuu katika mikoa ya Kigoma na Musoma/Mara.

Uboreshaji wa hali ya Wafanyakazi wa Mahakama; Hili pia ni moja kati ya eneo ambalo limepewa kipaumbele katika maboresho yanayoendelea kufanyika ndani ya Mahakama; Mhe. Jaji Mkuu aliwaeleza Watumishi wa Mahakama Mbeya kuwa uboreshaji huu unaangalia upatikanaji wa stahili za Watumishi kwa wakati ikiwa ni pamoja na nauli za likizo, madeni mbalimbali, uboreshaji wa mishahara ya watumishi suala ambalo linaendelea kufanyiwa kazi. 

Aidha Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kuwa suala Maadili na nidhamu pia limewekewa kipaumbele, alisema kuwa kuna baadhi ya Watumishi wa Mahakama hawana nidhamu na maadili katika utendaji kazi, hali hii imesababisha kuwa Mahakama nzima kutupiwa lawana juu ya utendaji kazi wake. 

“kuna baadhi ya Watumishi ya watumishi wa Mahakama hawana maadili na nidhamu hali hii inachafua taswira nzima ya Mahakama, lazima tuongeze uadilifu, Watanzania wanataka Watumishi wanaotoa haki, wanaoaminika ili kila mwananchi aridhike,” alisema.
Naibu Msajili, Mahakimu Wakazi Wafawidhi,Watendaji, Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala wa Kanda ya Mbeya waliokutana na kuzungumza na Jaji Mkuu wa Tanzania kuhusu utendaji kazi Mahakama kwa Kanda ya Mbeya.

No comments: