Saturday, April 30, 2016

CHRAGG yawapiga msasa Waandishi wa habari kuhusu Mpango wa Kimataifa wa Kujitathmini juu ya Masuala ya haki za binadamu.


Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu Umoja wa Mataifa, Chitralekha Massey akiwapiga msasa baadhi ya waandishi wa habari kuhusu Mpango wa Kimataifa wa Kujitathmini juu ya Masuala ya Haki za Binadamu (UPR) wakati wa warsha ya siku moja 29 Aprili 2016 Mkoani Morogoro.
Kamishna wa Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bi. Salma Ally Hassan (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu Mpango wa Kimataifa wa Kujitathmini juu ya Masuala ya Haki za Binadamu (UPR) wakati wa warsha ya siku moja 29 Aprili 2016 Mkoani Morogoro.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. James Jesse akitoa mada mbele ya waandishi wa habari kuhusu Mpango wa Kimataifa wa Kujitathmini juu ya Masuala ya Haki za Binadamu (UPR) wakati wa warsha ya siku moja 29 Aprili 2016 Mkoani Morogoro.



Afisa Utetezi na Haki za Binadamu wa Shirika la Under The Same Sun (UTSS) Bi. Perpetua Senkoro akitoa mada kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu kupewa haki zao wakati warsha ya siku moja kuhusu Mpango wa Kimataifa wa Kujitathmini juu ya Masuala ya Haki za Binadamu (UPR) wakati wa warsha ya siku moja 29 Aprili 2016 Mkoani Morogoro.




Wadau wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wakiwa katika picha ya pamoja na Waaandishi wa Habari waliohudhuria mafunzo ya siku moja ya warsha kuhusu Mpango wa Kimataifa wa Kujitathmini juu ya Masuala ya Haki za Binadamu (UPR) wakati wa warsha ya siku moja 29 Aprili 2016 Mkoani Morogoro.

(Picha zote na Benedict Liwenga)



Na Benedict Liwenga.


Asasi za Kiraia pamoja na Taasisi za kutetea haki za binadamu nchini zimewaasa Waandishi wa Habari nchini kujikita katika kuhabarisha umma kuhusiana na masuala ya haki za binadamu ikiwemo mauaji ya watu wenye ualbino, mauaji ya vikongwe, ukatili dhidi ya watoto, pamoja na adhabu ya vifo.

Rai hiyo imetolewa leo na Kamishna wa Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bi. Salma Ally Hassan wakati wa Warsha ya siku moja iliyofanyika mkoani Morogoro yenye lengo la kuwajengea uelewa Wanahabri kuhusu Mpango wa Kimataifa wa kujitathmini juu ya Masuala ya Haki za Binadamu (UPR).

Bi. Salma ameeleza kuwa kutokana na tathmini ya masuala ya haki za binadamu nchini, vyombo vya habari havinabudi kuwa na uelewa mkubwa kuhusu umuhimu wa kuziongelea haki za binadamu kwani jamii imekuwa haizitambui baadhi ya haki hizo na kumekuwepo na kukithiri kwa vitendo vya uvunjifu wa amani yakiwemo matukio ya mauaji ya watu wenye ualbino, vikongwe pamoja na ukatili kwa watoto.

Ameongeza kuwa, baadhi ya watu nchini wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi kwa kuua watu ambapo watu wenye kuyasemea hayo ni Vyombo vya Habari lengo likiwa ni kukemea kuendelea kwa vitendo hivyo.

“Uvunjaji wa haki za binadamu unafanywa na watu katika jamii, kwa mfano, mauaji ya Watu wenye Ualbino, mauaji ya vikongwe, pale sio Serikali inakua imevunja haki za binadamu, bali ni watu katika jamii”, alisema Bi. Salma.

Kwa upande wake Mshauri wa masuala ya haki za binadamu kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bi. Chitralekha Massey ameeleza kuwa, ni vema Tanzania ikakubalina na mapendekezo yanayohusiana na masuala ya haki za binadamu yanayoendana na Dunia kwa ajili ya ulinzi wa haki hizo.

“Sisi kama Umoja wa Mataifa tunapenda kuona Tanzania inafanya uamuzi utakaosaidia kuboreshwa kwa haki za binadamu nchini kwani ni wakati sasa wa jamii kusema kwa uwazi kuwa mapendekezo hayo yatakuwa yenye manufaa kwao”, alisema Massey.

Aidha, katika warsha hiyo, vyombo vya habari, jamii pamoja na Serikali wanajukumu la kulinda haki za binadamu na kuendelea kukemea matukio yanayovunja amani katika jamii.

Tarehe 9 Mei, 2016 Tanzania inatarajiwa kufanyiwa tathmini ya pili juu ya hali ya haki za binadamu nchini na Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa ambapo tayari Asasi za Kiraia na Watetezi wa haki za binadamu wamekwisha wasilisha mapendekezo yao kwa Wawakilishi wa nchi wanachama wa umoja huo.

No comments: