Tuesday, March 15, 2016

WAZIRI MKUU AMPA RAS KAGERA SIKU 5 AMLETEE TAARIFA


*Ni za matumizi ya sh. milioni 120 za Hospitali ya Mkoa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kagera na kumpa siku tano Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bw. Adam Swai amletee taarifa juu matumizi ya sh. Milioni 80 ambazo ni fedha za UKIMWI.

Pia amemtaka ifikapo Machi 20, nwaka huu awasilishe taarifa nyingine ya matumizi ya sh. Milioni 40 za ukarabati wa jengo la wagonjwa maalum  (Grade A)

Ametoa agizo hilo leo asubuhi (Jumanne,  Machi 15, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo baada ya kutembelea maeneo kadhaa yakiwemo wodi ya watoto, wodi ya wazazi, chumba cha wagonjwa mahututi (ICU ) na chumba cha kuhifadhia maiti.

"Kulikuwa na frsha za ukimwi sh. Milioni 80 ambapo kila mtumishi alipaswa kupata sh. 200,000/- lakini ninyi mmewapa sh. 80,000 /-. RAS fedha hizi zimeenda wapi?  Nataka uniletee taarifa ofisini kwangu Dar es Salaam ifikapo tarehe 20 mwezi huu," alisema huku akishangiliwa.

"Kwa mujibu wa taarifa ya CAG pale grade A kuna mgogoro wa sh. milioni 40. Wewe taarifa unayo lakini hujaifanyia kazi yoyote.  Nataka tarehe 20 nayo hii pia niipate na nione umetoa mapendekezo gani."

Kuhusu tatizo la madaktari katika hospitali hiyo, Waziri Mkuu alisema atawasiliana na Waziri wa Afya ili madaktari watano ambao wanasubiri ajira rasmi lakini wameanza kazi kwa mkataba hospitali hapo wapewe ajira rasmi. Pia alisema amebaini upungufu wa madaktari bingwa uliopo katika hospitali hiyo.

Pia aliahidi kufuatilia maombi yao ya gari la wagonjwa hasa ikizingatiwa kuwa anayo maombi kama hayo kutoka hospitali za Mawenzi (Kilimanjaro), na Ligula (Mtwara).
Katika hatua nyingine,  Waziri Mkuu aliwapongeza watumishi wa hospitali hiyo kwa huduma zao nzuri wanazotoa kwa wagonjwa.  "Nineridhishwa na kauli walizotoa wagonjwa juu yenu. Tofauti na hospitali nyingine nilizopita, wao wamesema hawajatozwa fedha ili wapatiwe dawa. Nimefarijika sana."

"Endeleeni kuwa na huruma kwa wagonjwa. Endeleeni kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa. Hawa wagonjwa hawakuogopa kuelezea hisia zao. Wamesema kwa uwazi kabisa kwamba mnawajali," alisema.

Mapema,  akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu,  Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk.  Thomas Rutachunzibwa alisema hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa madaktari bingwa pamoja na madaktari wa kawaida.

"Tunao madaktari 10 lakini wanaohitajika ni 30. Tunao madaktari wasaidizi wanane lakini wanaohitajika ni 23 na madaktari bingwa waliopo ni watatu tu lakini wanaohitajika ni 24. Tunaomba tupatiwe watumishi hawa ili tuweze kutoa huduma kulingana na matarajio ya wananchi wetu," alisema.

Akifafanua kuhusu mahitaji ya hospitali hiyo, Dk. Rutachunzibwa alisema wanahitaji sh. bilioni 1.8 kwa mwaka bila ya kuweka mishahara ili waweze kufanya kazi yao kwa umakini. "Tunahitaji sh. milioni 802 kwa ajili ya matumizi ya kawaida lakini tunachopokea hivi sasa ni sh. milioni 299 ambayo ni sawa na asilimia 30 ya mahitaji yetu."

"Bajeti ya dawa tuliyotenga ni sh. milioni 960 lakini tunapokea sh. milioni 143 ambazo kiuhalisia zinatosha kwa matumizi ya miezi miwili tu. Tumelazimika kufanya marekebisho ya bei za dawa kwa ridhaa ya Bodi ya hospitali ili tuweze kumudu kutoa huduma kwa wananchi," alisema.

Alisema ili kubana mianya ya upotevu wa mapato, wanahitaji kuwa na kompyuta 15 lakini hadi sasa wamefanikiwa kununua kompyuta mbili tu ambazo ziko Grade A na idara ya wagonjwa wa nje (OPD) ili kuimarisha utaratibu wa ukusanyaji mapato.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMANNE, MACHI 15, 2016.

No comments: