Thursday, March 3, 2016

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI AFANYA ZIARA MIKOA YA MARA NA MWANZA

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe. Inj. Gerson Lwenge amefanya ziara ya kikazi katika mikoa ya Mara na Mwanza leo na jana katika harakati ya kutatua kero ya maji kwa wananchi. Mhe. Lwenge ambaye ana dhamana ya kuinua na kuendeleza Sekta ya Maji na Umwagiliaji, amekagua miradi mbalimbali katika maeneo tofauti huku akizungumza na viongozi, wataalamu, wakandarasi na wananchi kwa nia ya kutafuta suluhisho la kudumu la tatizo ya maji.

Lengo kubwa la ziara hiyo ni kujua sababu ya kusuasua kwa utekelezaji wa baadhi ya miradi na kusukuma utekelezaji wa miradi inayotekelezwa katika mikoa hiyo ikamilike kwa wakati na kuleta matokeo mazuri kwa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla. Katika ziara hiyo Mhe. Lwenge alitembelea miji ya Musoma, Magu, Mwanza na Sengerema.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe. Inj. Gerson Lwenge, akiwa kwenye Mradi wa Kuzalisha na Kusambaza Majisafi wa Musoma Mjini ambao utekelekezaji wake utagharimu Sh. Bil 45 ambao unategemewa kukamilika Juni, 2016 na unategemewa kutoa huduma ya maji katika Manispaa ya Musoma kwa zaidi ya asilimia 90.
Mtambo wa Kusafisha na Kutibu Maji ambao ni moja ya sehemu ya Mradi wa Kuzalisha na Kusambaza Majisafi wa Musoma Mjini ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 75 kwa sasa.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe. Inj. Gerson Lwenge akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa tanki la Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) lenye mita za ujazo 135,000 eneo la Rwamlimi, Halmashauri ya Manispaa ya Musoma ambalo linategemewa kuhudumia wakazi 1,000.
Mradi wa Maji wa Lugeye-Kigangama, Magu, mkoani Mwanza ambao unatekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ukiwa katika hatua za ukamilishaji, ambao unatarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 11,000 utagharimu zaidi ya Sh. bilioni 1.
Sehemu ya Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira mjini Sengerema LV WATSAN II, eneo la Nyamazugo ambao utekelezaji wake umeanza Oktoba, 2014 na unategemewa kukamilika Juni, 2016 unatarajiwa kuhudumia wakazi 93, 267 sawa na asilimia 100 ya wakazi wote waishio Sengerema na vijiji jirani vinavyopitiwa na mradi huu.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhe. Inj. Gerson Lwenge akiwa na Mkuu wa Wilaya wa Sengerema, Zainab Tulack (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Mwanza (MWAUWASA), Inj. Anthony Sanga (kulia) kwenye Tenki la Maji ambalo ni sehemu ya Mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Sengerema LV WATSAN II.

No comments: