Sunday, March 6, 2016

CRDB Yajivunia Mafanikio YA Miaka 20 Kwa Kutimiza Malengo ya Kufikisha Huduma Vijijini

Benki ya CRDB inajivunia mapinduzi makubwa katika sekta ya fedha nchini, iliyoyafanya katika kipindi cha miaka 20 ya uwepo wake, kwa kufanikisha kuwafikishia huduma za kifedha Watanzania walio wengi na haswa walio vijijini, hivyo CRDB kujikuta imetimiza malengo ya kuanzishwa kwake. 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dr. Charles Kimei, katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hizi, katika kutathimini mafanikio ya benki ya CRDB kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya Benki ya CRDB.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dr. Charles Kimei, akifanya mahojiano maalum na Mwandishi wa Habari wa Kujitegemea, aliyejikita katika kuandika habari za kimaendeleo, Pascal Mayalla, kuhusiana na maendeleo yaliyoletwa na CRDB Banki katika kipindi cha miaka 20.

Dr Kimei amesema, miongoni mwa mafanikio makubwa ya kujivunia ya Benki ya CRDB, ni kitendo cha benki hiyo kufanikiwa kutimiza malengo, dira na dhima ya benki hiyo, ambayo ni kufikisha huduma za kibenki kwa Watanzania wengi zaidi hadi vijijini, ambapo lengo hili limetizwa kupitia kwa mawakala wa CRDB waitwao Fahari Huduma waliotapakaa nchi kote hadi Vijijini.

“Katika mambo mengi ambayo CRDB inajivunia katika miaka hii 20, ni kuingiza mfumo mpya wa kimapinduzi wa kutolea huduma kwa wateja wetu wengi zaidi hadi wa hali ya chini ambao wengi wako vijijini, wamekuwa hawafikiwi na huduma za kibenki, hivyo Lengo na azma ya CRDB ya kuwafikia wateja wengi, limetimizwa. 
Akinamama wa Kibamba, wakielekea kwenye kituo cha Wakala wa Fahari Huduma wa Kibamba, kupata huduma za kifedha, wakala huo, unaomilikiwa na Bw. Frank Mwalinga na mkewe Mainda, wakati wa ziara za kukagua mafanikio ya miaka 20 ya Benki ya CRDB.

Akielezea mafanikio ya jumla ya CRDB Bank ndani ya miaka ishirini ya kutekeleza dira, dhima na Mipango Mikakati iliyoshabihiana na dira hiyo, Dr. Kimei amesema, Mtandao wa CRDB, una matawi 198, unaojumuisha vituo mbadala vya kutolea huduma kwa wateja zikiwemo ATMs 461, vituo vya Wakala wa Fahari Huduma 1800, Vituo vya kutoa huduma kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa 40, SACCOs zilizoingia ubia na Kampuni Tanzu ya CRDB Microfinance Services, 482, na Vifaa vya kutolea huduma kwenye vituo mbalimbali vya biashara kama vile mahoteli, supermarkets, mahospitali 989.

Akizungumzia mafanikio mengine ya miaka 20 ya CRDB Bank, Dr. Kimei amesema CRDB Banki ina wateja 1,800,000, wenye amana za zaidi ya shilingi trilioni 4.2. ambapo CRDB Bank imetoa mikopo ya shilingi trilioni 3.3 na kwa sasa ina jumla ya raslimali za trilioni 5.3.

Pia Dr. Kimei, amezungumzia baadhi ya huduma ambazo CRDB Bank imekuwa ya kwanza kuzianzisha, CRDB Bank imekuwa ni benki ya kwanza kuunganisha matawi yake nchi nzima na kufanya kazi kama tawi moja na hivyo kuwezesha uhamishaji wa fedha kutoka tawi moja kwenda jingine papo kwa papo tangu mwaka 1999. CRDB Banki imekuwa ya kwanza kuanzisha mfumo wa kutoa huduma kwa wateja wake kwa kutumia kadi za ATM mwaka 2002: Hadi leo CRDB ina kadi za Visa na Mastercard zinazofikia 1,400,000 

CRDB Bank ndio benki ya kwanza kubuni bidhaa inayokidhi mahitaji ya watoto (Junior Jumbo Account) na wanafunzi (Scholar Account) ambazo leo hii mabenki yote yameiga. CRDB Bank ndio ya kwanza kuingiza bidhaa mahsusi ya uwekezaji inayolenga Wanawake—Malkia Account na imekuwa benki ya kwanza kuona fursa katika kuwapelekea huduma za kibenki kwa watanzania wanaoishi nchi za nje: Akaunti yenye chapa ya Tanzanite.
Dr. Kimei amesema haya yote yamewezekana kwa timu ya wafanyakazi 2,682 wanaofanya kazi kwa bidii, ubunifu na kujituma na ari ya hali ja juu.

Akichangia mafanikio haya ya CRDB, Meneja Mkuu wa CRDB Microfinance Services Company Ltd, Bw. Sebastian Masaki, amesema CRDB imeyaweza yote hayo kutokana na juhudi za kuhakikisha inasaidia kupunguza ukosefu wa huduma za kibenki kwa Watanzania walio wengi, haswa waishio vijijini au mbali na matawi ya taasisi za kifedha. Hivyo lengo kubwa la CRDB ni kutafuta njia mbadala za kuwafikishia wananchi huduma za kifedha karibu na mahali walipo, ndipo ikabuni kuwatumia mawakala wa fahari huduma ambao wako zaidi ya 1800 na wamesambaa nchi nzima.
Wageni mbalimbali wakitembelea Wakala wa Fahari Huduma wa Kibamba, kushuhudia mafanikio ya miaka 20 ya Benki ya CRDB. wakala huo, unaomilikiwa na Bw. Frank Mwalinga na mkewe Mainda.
Akinamama wa Kibamba, wakimpokea kwa furaha, Mkuu Oparations wa CRDB Microfinance, Bw. Samson Keenja, alipokwenda kutembelea Wakala wa Fahari Huduma wa Kibamba, unaomilikiwa na Bw. Frank Mwalinga na mkewe Mainda, wakati wa ziara za kukagua mafanikio ya miaka 20 ya Benki ya CRDB.



Meneja Mkuu wa Kampuni ya CRDB Micofinance, ambayo ni kampuni Tanzu ya Benki ya CRDB, Bwana Seabastian Masaki, akifanya mahojiano maalum na Mwandishi wa Habari wa Kujitegemea, aliyejikita katika kuandika habari za kimaendeleo, Pascal Mayalla, kuhusiana na maendeleo yaliyoletwa na CRDB Banki katika kipindi cha miaka 20 ambapo kampuni hiyo ya CRDB Microfinance ni moja ya vielelezo vya mafanikio hayo.

No comments: