Saturday, March 19, 2016

Barabara za DART DSM – Alama zinahitaji kuboreshwa

Kama umekua nje ya Jiji la Dar es Salaam kwa muda mrefu, ni wazi kwamba ukija utahitaji kupata maelekezo ya mambo kadha wa kadha ili kurahisisha maisha na shughuli zako kwani kuna mabadiliko ya vitu vingi. 

Pamoja na badiliko kubwa la UTUMBUAJI MAJIPU ambalo liko kinywani mwa kila mtu unayekutana naye, kuna mabadiliko ya matumizi ya barabara hasa zile ambazo zinatarajiwa kutumika kwa mabasi yaliyolenga kuboresha usafiri wa umma. Barabara hizi (hasa Morogoro na Kawawa) zimekua safi zaidi; zimekua nyembamba ukilinganisha na awali; zimeongezwa taa za kuongoza magari; na zina alama mpya/za ziada. 

Kama vile haitoshi, maboresho ya barabara hizi yamebadili mwelekeo wa baadhi ya safari kwani kuna maeneo huruhusiwi tena kukata kulia au kushoto; kuna maeneo huwezi kuingi kwenye barabara za pembeni; na kwingine unalazimika kuchepuka na kupita njia za pembeni ili kupata barabara kuu.



Kwa wengi ambao hatujaendesha magari nje ya nchi yetu au kwenye nchi zenye barabara za kisasa zaidi, mabadiliko haya ni makubwa na huenda yakatuchanganya. Kuna baadhi ya alama nimeziona sijawahi kuziona sehemu nyingine yoyote Tanzania na hata shule za driving hazikua zinafundisha maana hazikua na matumizi kwenye barabara tulizonazo. Kwa mfano, kwenye nchi zilizo na barabara za kisasa, wana alama nyingi zaidi ikiwa ni pamoja na alama zinazokuonesha kwamba kwenye barabara unayopita huruhusiwi kusimama (isipokua kwa immergency pekee) au unaruhusiwa kusimama kwa lengo maalumu lakini huruhusiwi kungoja au kupaki. Kwa mara ya kwanza, alama hizi zinaonekana kwenye barabara zilizoboreshwa.
Pamoja na maboresho haya ambayo ni wazi kwamba ni hatua moja mbele katika upanuaji na uboreshaji wa barabara zetu kuwa za kisasa zaidi, bado kuna tatitizo la msingi katika matumizi ya alama za barabarani kwa lengo la kumsaidia mtumiaji. Kwa uchambuzi wangu wa haraka baada ya kupita kwenye barabara hizi, nimeona shida kadhaa:


1. Alama za barabarani zilizowekwa pamoja na maandishi yanayoendana nazo, ni ndogo sana. Pamoja na ukweli kwamba barabara zetu zimepakana na “mbwembwe” za kila aina, inahitahi umakini mkubwa kuziona na kuzielewa.

2. Alama nyingi za barabarani zimewekwa karibu sana na mahali ambapo zinahitajika na hivyo kumpa dereva muda mfupi sana wa kuzitafakari na kuzielewa kabla ya kuchukua hatua

3. Alama nyingi za muhim zimewekwa mara moja tu. Kwa mfano, unapokaribua makutano ya Morogoro na Kawawa, kuna mbadiliko ya jinsi ya kupita kwa wanaoelekea barabara ya Kawawa kutoka Morogoro na kinyume chake. Hata hivyo, alama inayokupa maelekezo ya kupita (kama nimeona vizuri) iko moja tu kuanzia huko unakotoka na iko karibu kabisa na mahali pa kuchukua maamuzi

4. Alama za barabarani zimewekwa kwenye vibao tu na hakuna maandishi yoyote yaliyoandikwa chini (kwenye njia) kumsaidia dereva kuelewa zaidi na kuepuka makosa

Iwapo barabara hizi zitawekwa alama zote muhim kwa ukubwa, nafasi, na ubora unaotakikana, itarahisisha sana usalama wa watumaiji na kuzuia makosa yasiyo ya lazima kwa madereva. Pia zitasaidia kutotumika nguvu kubwa kuwinda wakosaji na badala yake muda wa askari utatumika kwa kazi nyingine muhim za ulinzi na usalama wa raia. Alama hizi zinapokuwa wazi na za kutosha, zinasaidia kuiweka sawa saikolojia ya madereva na kujikuta wanalazimika kufuata sheria na kanuni bila shuruti.

NB: Maoni haya ni mtazamo wangu kwa kile nilichojionea kwenye barabara hizi. Inawezekana kuna ambavyo sijaona na hivyo kutokua sahihi kwa 100% katika yale niliyoshauri.

Mtumiaji wa Barabara.

Mwalimu MM (mmmwalimu@gmail.com


No comments: