Tuesday, February 16, 2016

WAZIRI MBARAWA ASISITIZA UKUSANYAJI WA MAPATO KATIKA SEKTA YA MIUNDOMBINU

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiongea na mkandarasi Nyanza Road Works anayejenga barabara ya Bulyamba-Kisolya yenye urefu wa Km 51. (Wa kwanza kushoto) ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda Bw. Joshua Mirumbe.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kisolya kuhusu ujenzi wa mradi wa barabara ya Bulyamba-Kisolya yenye urefu wa Km 51 inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Muonekano wa barabara ya Bulyamba-Kisolya yenye urefu wa Km 51 inayojengwa kwa kiwango cha lami ambayo ni sehemu ya barabara ya Nyamuswa-Bunda hadi Nansio Km 121.9.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Meneja wa wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Eng. Emmanuel Koroso (wa pili kulia) wakati akikagua daraja la Kyarano linalounganisha barabara ya Makutano-Nata- Mto wa Mbu yenye urefu wa Km 467.7.
Muonekano wa daraja la Kyarano linalounganisha barabara ya Makutano-Nata- Mto wa Mbu yenye urefu wa Km 467.7 likiwa katika hatua za ujenzi.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiongea na watumishi wa sekta za Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (hawapo pichani) kuhusu kufanya kazi kwa umoja na kuongeza mapato katika sekta zao, mkoani Mara.
Meneja wa uwanja wa ndege wa Musoma Bi. Bertha Bankwa akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa katika mkutano wa watumishi wa sekta zilizo chini ya Wizara hiyo.
Daraja la reli linaloingia baharini katika bandari ya Musoma kupokea na kupakia mizigo kwenye melikwa ajili ya kuisafirisha katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewataka watendaji walio chini ya Wizara yake kuongeza kasi ya kukusanya mapato ili kuwezesha malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi kufikiwa kwa wakati.

Akizungumza na watumishi wa sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino mjini Musoma, Prof. Makame Mbarawa amesema kufanya kazi kwa umoja, uadilifu, uwazi na ubunifu kutasababisha kufikiwa kwa malengo hayo mapema.

“Kama mtu hawezi kufanya kazi kwa kasi na kwa malengo yanayotekelezeka na kupimika atupishe kabla hatujamuondoa, hatuta muonea mtu na hatutamvumilia mtu atakayeshindwa kuendana na kasi yetu”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amesema Serikali imetenga zaidi ya dola milioni 30 kwa ajili ya kukarabati uwanja wa ndege wa Musoma na kununua magari ya kisasa ya zimamoto ili kurudisha hadhi ya uwanja huo.

Aidha, amezitaka taasisi za Serikali zinazodaiwa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoani Mara kulipa madeni yao ili kuuwezesha wakala huo kufanya kazi kwa kasi na kufikia malengo yaliyowekwa.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Makutano-Nata-Mto wa Mbu yenye urefu wa km 467.7 inayojengwa na makandarasi wazalendo kumi na kutaka mkandarasi anayejenga kipande cha km50 kutoka Makutano hadi Sanzate kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa haraka ikiwemo daraja la kyarano ili kuiwezesha barabara hiyo kupitika wakati wote wa mwaka.

Amemwagiza Meneja Wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa Mara Eng. Emmanuel Koroso kuhakikisha makandarasi wanaojenga barabara mkoani humo wanarejea kazini kwa kuwa serikali imeanza kulipa madai yao.

Ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kutumia fedha zilizotumwa kutoka Mfuko wa Barabara (RFB) kutumika kwa miradi iliyokusudiwa ili kuingunisha wilaya hiyo mpya na wilaya nyingine mkoani Mara kwa barabara za lami.

Akiwa wilayani Bunda Prof. Mbarawa amemtaka mkandarasi Nyanza Road Works anayejenga barabara ya Buliamba-Kisolya Km 51 kuendelea na ujenzi wa barabara hiyo kwa mujibu wa mkataba kwani serikali imeshalipa fedha shilingi bilioni 8.5 kwa ajili ya barabara hiyo ambayo ni sehemu ya barabara ya Nyamuswa-Bunda-Kisolya-Nansio yenye urefu wa Km 121.9.

Aidha, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Mbarawa amewataka viongozi wa Wilaya za Magu, Bunda na Musoma kufanya kampeni kubwa ya kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kulinda Miundombinu ya Barabara, Reli na Mkongo wa taifa wa Mawasiliano ili isihujumiwe na kusababisha usumbufu kwa jamii na kuisababishia serikali hasara.

Naye, Mbunge wa Mwibara Mhe. Kangi Lugola amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa kukamilika kwa barabara ya Nyamuswa-Bunda-Kisolya hadi Nansio yenye urefu wa KM 121.9 itasaidia kukuza uchumi wa Wilaya ya Bunda na Ukerewe kwa kuwa eneo hilo lina shughuli nyingi za uchumi zinazotokana na kilimo, ufugaji na uvuvi wa Samaki.

Prof. Mbarawa amewataka makandarasi wote nchini kuhakikisha wanawapa wafanyakazi wao mikataba kulingana na sheria za nchi ili kuwezesha miradi ya barabara inayoendelea kujengwa kukamilika kwa wakati na kuondokana na hujuma zinazoweza kudhoofisha ujenzi wa barabara na miundombinu mingine.

“Lindeni miundombinu ili idumu kwa muda mrefu, barabara, reli na mkongo wa taifa ni miongoni mwa miundombinu inayojengwa kwa fedha nyingi na kuhujumiwa mara kwa mara hivyo kuisababishia Serikali hasara”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa yupo kwenye ziara ya kukagua Ujenzi wa miundombinu ya barabara, bandari na mkongo wa taifa wa mawasiliano katika mikoa ya kanda ya ziwa ambapo ametembelea Wilaya za Magu, Bunda, Butiama na Musoma.

No comments: