Monday, February 15, 2016

Siku 100 za JPM Usafi wapewa kipaumbele.

Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Mnamo tarehe 5 Novemba 2015 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilishuhudia Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano katika sherehe zilizofanyika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam. Huu ndio ulikuwa mwanzo mpya wa Tanzania ya uwajibikaji na maendeleo ya mtu wa hali ya chini ambayo watanzania wengi walisubiri kwa muda mrefu vizazi na vizazi kuiona.
Siku 100 tangu Rais wa awamu ya tano aiingie madarakani mambo mengi yametiliwa mkazo kama vile Elimu, Afya, Biashara, Viwanda,Kilimo,Ufugaji,Uvuvi na mengine mengi ambayo serikali imeamua kuyaangalia kiundani zaidi ili kufanikisha azma yake ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Katika makala hii tuangalie jinsi uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano katika siku 100 ulivyojikita  kuimarisha usafi wa mazingira ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko yanayotokea mara kwa mara katika mikoa mbalimbali nchini kwa kuhamasisha usafi katika maeneo hayo. Hapa tunamsikia Mhe. Rais John Pombe Magufuli akisema, “Hatuwezi kufanya sherehe huku watu wetu bado wanakufa kwa ugonjwa wa kipindupindu ambao unatokana na uchafu, badala yake nchi nzima tufanye usafi siku hiyo”.
Kwa kuliona hilo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alitangaza rasmi kuwa siku ya tarehe 9 Desemba mwaka 2015, itakuwa ni siku ya uhuru na kazi na maadhimisho ya miaka 54 ya  Uhuru wa Tanganyika  kuwa yatafanyika kwa watu kufanya usafi katika maeneo yao siku hiyo, ikiwa ni jitihada za Serikali kuimarisha usafi na kupambana na magonjwa ya mlipuko kama vile Kipindupindu.
Kero ya uchafu ilimfanya Mhe. Rais kufanya tendo la kihistoria ambalo halijawahi kufanyika kwa takribani zaidi ya nusu karne ya uhai wa Tanzania. Tukio hili ni kuhamisha maadhimisho tuliozoea ya kuona gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na halaiki na lakini sasa tunashuhudia machepe, troli, ndoo, fyekeo na zana nyinginezo za usafi zikitumika siku hiyo. Ama kweli Dr. Magufuli ni kiongozi mwenye uthubutu.
Katika kufanya usafi kama maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanganyika,  Rais John Magufuli aliongoza kwa vitendo zoezi la kufanya usafi  kama alivyoelekeza baada ya kufuta shamrashamra za maadhimisho ya siku ya Uhuru, Desemba 9.  Rais Magufuli na mkewe Janeth Magufuli walifanya usafi katika maeneo ya Feri, eneo ambalo liko mita kadhaa kutoka Ikulu Jijini Dar es Salaam naye Makamu wa Rais, Samia Suluhu yeye alionekana akifanya usafi katika eneo la ufukwe wa Bahari wa ‘Coco Beach’na baadae kuelekea maeneo ya Kinondoni Morocco Jijini Dar es Salaam. Katika maadhimisho hayo,   Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa aliunagana na wananchi kufanya usafi katika maeneo ya Kariakoo Jijini Dare s Salaam. Wizara,Taasisi ,Idara,Wakala wa Serikali ,mashirika binafsi Asasi zisizo za kiserikali, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao walishiriki kufanya usafi katika maeneo mbalimbali katika kutimiza agizo la kuifanya siku ya 9 Desemba iwe ya kufanya usafi.
Baada ya Rais kushiriki katika kufanya usafi,wananchi wengi walipata mwamko wa kufanya suala la usafi kuwa ni moja ya utaratibu wao wa kila siku katika maeneo yao hata kwa baadhi ya sehemu kutangaza baadhi ya siku kuwa ni siku rasmi za kufanya usafi katika maeneo yao na hatimaye Naibu Waziri wananchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luaga Mpina alitangaza kuwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi itakuwa siku rasmi ya kufanya usafi wa mazingira ili kupambana na magonjwa yanayosababishwa na uchafu kama vile kipindupindu.
Katika kulilipa nguvu swala kuimarisha mazingira kwa kuzingatia usafi katika maeneo mbalimbali,Halmashauri za Majiji ,Wilaya na  Miji zilianzisha faini kupitia sheria ndogo ndogo zilizopo ili kupambana na uchafuzi wa mazingira unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya watu, na kwa kuanza Halmashauri ya Manispaa ya wilaya ya Ilala ilitangaza rasmi kwa yoyote atakayekamatwa anatupa taka sehemu isiyostahili atatozwa faini ya shilingi elfu 50 taslimu na kutangaza kutoa nusu ya fedha ya faini kama zawadi kwa kuwahamasisha wananchi kutoa taarifa au kufanikisha kukamatwa kwa mtu atakayevunja Sheria hiyo.  
Kamapeni za usafi zilifanyika katika Mikoa,Wilaya ,Miji na Vijiji nchi kote kwqa wananchi kushirika katika kufanya usafi na kufanya usafi kuwa ni utamaduni wao na sio mpaka litolewe tamko juu ya kusafisha mazingira yanayowazunguka, katiak kampeni hii ya usafi siku ya 9 Desemba ilikubwa na baadhi ya changamoto ikiwa baadhi ya wananchi kutoshiriki kampeni hizo katika maeneo yao na kuwepo kwa uhaba wa magari ya kuzolea taka katika Halmashauri za Majiji, Wilaya na Miji iliy osababisha taka kukaa kwa muda mrefu katika baadhi ya maeneo lakini juhudi toka Halmashauri hizo zilifanyika na kuwezesha kuzolewa na kutupwa katika madampo husika.
Katika kutekeleza suala la kuimarisha usafi wa mazingira Serikali kupitia Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na watoto kupitia waziri wake Mhe. Ummy Mwalimu ilitoa tamko la kupiga marufuku uuzwaji wa vyakula ovyo katika maeneo yasiyo rasmi na ya wazi na uzwaji wa matunda yaliyokatwa ikiwa ni jitihada za Serikali kupambana na wafanyabiashara wasiozingatia kanuni za usafi na Afya ambazo zinaweza kuhatarisha afya za walaji wa vyakula hivyo ikiwemo mlipuko wa magonjwa kama Kipindupindu.
Kampeni hizo za usafi siku ya 9 Desemba zilileta mafanikio makubwa katika jamii ya watanzania hususani  kuhamasisha tabia ya kufanya usafi katika maeneo yao ili kuweka mazingira safi na pia kupambana na magonjwa ya mlipuko.Katika kuweka mazingira safi makampuni mbalimbali yaliunga mkono agizo la Mhe Rais la kufanya usafi siku ya 9 Desemba na kushiriki katika usafi katika maeneo mbalimbali nchini.
Baadhi ya makampuni yaliyoshiriki katika kufanya usafi siku hiyo ya Uhuru wa Tanganyika ni pamoja na Clouds Media Group, Msalaba Mwekundu, Max Malipo, NSSF, Benki ya Biashara ya Akiba (ACB), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kliniki ya Tiba Mbadala ya Ifakara Herbalist Clinic waliofanya usafi katika soko la Tandale., Wwengine ni Mohamed Enterprises Group MeTL Benki ya FNB waliofanya usafi ufukwe wa Coco,GEPF na kampuni ya Saruji ya DANGOTE walifanya usafi soko la Mbae Mkoani Mtwara, Airtel Tanzania ilifanya usafi Hospitali ya Wilaya ya Nzega Tabora, kampuni ya PUMA ilishiriki na kutoa vifaa vya usafi katika Manispaa ya Temeke na Azania Bank nayo ilitoa vifaa vya usafi na kushiriki usafi katika Halmashauri ya Mji wa Moshi.
Juhudi zimefanya Wizara inayohusika na Mazingira kwa kushirikiana na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa kufanya usafi katika mazingira ili kujenga tabia ya kuweka mazingira safi na kujiweka mbali na magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na uchafu.
Haya shime Watanzania tumuunge mkono Rais wetu kwa kuufanya usafi kuwa ni tabia katika maisha ya kila siku ingawa kuna changamoto mbalimbali zinazokabili  maeneo yetu zikiwemo Halmasahuri za Majiji,Wilaya na Miji katika kutatua changamoto hizo,hivyo basi hatuna budi kushirikiana na Serikali ya Rais Magufuli kuboresha mazingira yetu kwa kufanya usafi kwa faidi yetu na vizazi vyetu.




No comments: