Thursday, February 4, 2016

SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR IMEAMUA KUANZISHA UTARATIBU WA KUTUMIA NJIA YA UPANDE MMOJA.

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mjimkongwe Issa Said Makarani akizungumza na waandishi wa habari pichani hawapo juu ya kutumia njia moja ya kuingilia Mjimkongwe kuanzia tarehe 8/2/2016.
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Mkadam Khamis Mkadam akizungumzia namna Jeshi la Polisi lilivyojipanga kuhakikisha Wananchi wananchi wanafuata sheria zitakazowekwa na Mamlaka ya Mjimkongwe kuanzia Februari 8 mwaka huu.
  Mkurugenzi Mipango Miji Dokta Moh’d Juma akijibu maswali kutoka kwa Waandishi wa habari (hawapo pichani) katika mkutano wa kutoa taarifa ya njia moja ya kuingilia Mjimkongwe kuanzia Februari 8 mwaka huu.
 Mkurugenzi wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Aboud Hassan Serenge akielezea mashirikiano waliyonayo na Mamlaka ya Mjimkonge katika kuimarisha matumizi ya njia ya Mjimkongwe ifikapo tarehe 8/2/2016.
 Mwandishi wa Habari wa Coconut FM Tabia Makame akiuliza maswali kuhusu zoezi zima la utumiaji wa Njia hiyo na namna wananchi watakavyoepuka usumbufu katika Mjimkongwe.Picha na Abdalla Omar Habar-Maelezo Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Mji Mkongwe Issa Said Makarani akijibu masuala ya waandishi wa habari.

Mwashungi Tahir Maelezo 4-2-2016.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kuanzisha utaratibu wa kutumia njia ya upande mmoja kubwa ya kuingia Mji Mkongwe kuanzia tarehe nane mwezi huu ili kupunguza usumbufu unaowapata wageni na watumiaji wengine wa Mji huo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mamlaka ya Mji Mkongwe Forodhani, Mkurugenzi Mkuu Issa Saidi Makarani amesema uwamuzi huo umefikiwa kutokana na ongezeko kubwa la vyombo vya moto linalohatarisha usalama wa mji huo ambao ni urithi wa kimataifa.

Amesema mji wa Zanzibar umekuwa ukipokea watalii na wageni wengi na wakati wa matembezi yao wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa kutokana na kuongezeka vyombo hivyo.

Ameongeza kuwa ongezeko hilo la magari pia limepelekea athari kubwa kwenye majengo kutokana na mtikisiko mkubwa wa magari yenye uzito mkubwa na kubomoa baadhi ya majengo ya mji.

“Watumiaji wa Mji huu na wanaofika kila siku kwa shughuli zao za kimaisha wanapata usumbufu na kubwa zaidi wingi wa vyombo hivyo tayari vimesababisha athari ya baadhi ya majengo,”alisisitiza Mkurugenzi Makarani.

Amesema njia kubwa ya ndani ya kuingilia Mji Mkongwe itaanzia Vuga kupitia Afrika House , Hoteli ya Serena , Wizara ya Ardhi , Makaazi, Maji na Nishati , Benki ya NBC , Jengo La zamani la Watoto Forodhani , njia ya Mizingani hadi kuishia lango kuu la kuingia bandarini Malindi.

Amezitaja njia zitakazofungwa kuanzia tarehe nane kuwa ni ile inayoanzia jengo la Wizara ya zamani ya Mawasiliano na Uchukuzi kupitia Kiponda na kumalizikia Darajani, njia inayoingia Mkunazini na kumalizikia Skuli ya Sunni Madrassa na njia inyozunguka nyuma ya jengo la sinema ya zamani Majestic.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Mkadam Khamis amesaema lengo la kuweka zoezi hilo ni kuweka usalama kwa wenye magari na wanaokwenda kwa miguu.

Amewaomba wananchi kuunga mkono zoezi hilo ambalo litaweka mji Mkongwe katika hadhi na ubora wake uliopelekea kuwa miongoni mwa Miji ya Urithi wa kimataifa duniani.




Mkurugenzi wa Baraza la Manispaaa Aboud Hassan Serenge amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo ya Mji Mkongwe kubadilika na kuanzisha utamaduni wa kuimarisha suala la usafi.

No comments: