Thursday, February 18, 2016

MADIWANI WAPITISHA MAPENDEKEZO YA KUBADILI MATUMIZI YA MIL.40 ZA VIBURUDISHO KUPELEKWA SEKONDARI ZA WASICHANA

Na Jumbe Ismailly,Singida

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Singida limepitisha mapendekezo ya kufanyika kwa mabadiliko ya matumizi ya zaidi ya shilingi milioni 40 zilizotengwa kwa ajili ya kununua viburudisho na vitafuno wakati wa vikao mbali mbali vya Halmashauri hiyo na badala yake fedha hizo zielekezwe katika kutatua matatizo yaliyopo katika shule za sekondari za bweni kwa wasichana.

Diwani wa kata ya Ikhanoda,Hinga Mnyawi alitoa mapendekezo hayo kwenye mkutano maalumu wa Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo uliokutana kwa lengo la kupitisha mwelekeo wa mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017 uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Singida wakiwa katika mkutano wa kupitisha mapendekezo ya mwelekeo wa bajeti ya halmashauri hiyo ya singida vijijini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Singida, Simon Mumbee akipitia taarifa zake anazotarajia kuwasilisha kwenye mkutano huo maalumu kwa ajili ya kupitisha mapendekezo ya mwelekeo wa bajeti ya 2016/2017.

“Jingine mwenyekiti wakati afisa elimu sekondari akituaga amenikuna sana lakini sisi naye tuliangalie sana hili,tunatenga fedha kwa ajili ya viburudisho pamoja na vitafuno zaidi ya shilingi milioni arobaini nimesoma hapa,zile hela kwa nini badala ya kula hapa tuzielekeze ziende kuwasaidia watoto wa kike wanaosoma katika shule za bweni”alisisitiza Mnyawi.

Aidha diwani huyo alizitaja shule zitakazonufaika na kiasi hicho cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya viburudisho na vitafuno kuwa ni pamoja na Kijota,Ughandi,Msange,Ikhanoda na Mwanamwema zilizopo katika Halmashauri hiyo.

Hata hivyo Mnyawi alibainisha kuwa umefika wakati kwa Halmashauri hiyo kulipa deni la Kituo cha afya kilichojengwa katika Kijiji cha Ngimu kwa zaidi ya miaka saba sasa lakini bado halijaezekwa.  

Baadhdi ya wakuu wa idara wa halmashauri ya wilaya ya singida vijijini wakiwa katika mkutano wa kupitisha mapendekezo ya mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2016/2017.

Kwa mujibu wa diwani huyo wakati wa kuanza ujenzi wa kituo hicho wananchi walingia mkataba na mkandarasi kwa makubaliano ya kumlipa shilingi milioni arobaini mara ujenzi huo utakapokamilika,jambo ambalo wameshindwa kutekeleza.

“Kwenye ukurasa wa kumi inasema uwepo wa madeni katika miradi viporo nakumbuka kuna kituo cha afya kata ya Ngimu wananchi waliingia mkataba na mkandarasi kwa makubaliano ya shilingi milioni arobaini kazi itakapokamilika,lakini mpaka sasa bado hazijalipwa.”alibainisha Mnyawi.

Aidha diwani Mnyawi hata hivyo aliweka bayana kwamba katika kudhihirisha kwamba ujenzi wa zahanati hiyo umesahaulika aligundua kwamba hata kwenye kabrasha walilokabidhiwa kujadili mwelekeo wa mpango wa bajeti ya mwaka ujao wa fedha hakuna sehemu inayolitamka jengo hilo.
Diwani magreth Mangu (wa kwanza kutoka kulia) akibadilishana mawazo muda mfuppi baada aya kumalizika mkutano maalumu wa baraza la madiwani kupitissha mapendekezo ya mwelekeo wa bajeti ya Halmashauri hiyo ya mwaka 2016/2017.

Wakichangia hoja ya mwelekeo wa mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017 baadhi ya madiwani wa Halmashauri hiyo walionyesha wasiwasi wao juu ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara.

Kwa mujibu wa diwani wa kata ya Merya,Iddi Kijida kiasi cha shilingi milioni 39 zilizotengwa kwa ajili ya barabara yenye urefu wa zaidi ya kilomita 45 haziwezi kukamilisha matengenezo ya uhakika wa kuwawezesha wananchi wanaolima na kusafirisha mazao ya biashara kama vitunguu kwenda kuuza mazao yao kwenye soko la mjini Singida.

Naye diwani wa kata ya Itaja,Paul Himida aliweka bayana kwamba kutokana na Halmashauri hiyo kuwa na mahitaji makubwa ya fedha hivyo hawana budi kwenda kusimamia kwa karibu makusanyo ya ndani ili waweze kufanikisha kusaidia kwenye miradi viporo vilivyobakia katika mwaka wa fedha wa 2015/2016.
Katibu wa CCM wilaya ya singida vijijini,Bi Mwamvua Killo(wa kwanza kutoka kulia) akisalimiana na baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya wilayaa ya singida mara tu mkutano huo ulipomalaizika.

Akifungua mkutano huo maalumu wa Baraza la madiwani,Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Singida,Elia Dgha alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi juu ya umuhimu wa kuzitumia mvua zinazoendelea kunyesha wakati huu kwa kulima mazao ya mzizi ikiwemo viazi na mihogo,mtama na uwele kwa mazao ya chakula na alizeti na vitunguu kwa biashara yatakayowasaidia endapo baa la njaa litawakumba kama ambavyo lilivyowakumba kwa mwaka wa 2015/2016.

Hata hivyo Digha ambaye pia ni diwani wa kata ya Msange aliishukuru serikali kwa kuipatia Halmashauri hiyo zaidi ya tani mia nne za chakula ambazo zimewasaidia wananchi wake kukabiliana na upungufu wa chakula uliokuwa ukiwakabili.

No comments: