Friday, February 12, 2016

JENGO LA HOSTELI CHUO CHA MADINI LAKAMILIKA

 Mkuu wa Chuo cha Madini cha Dodoma, Mhandisi Oforo Ngowi (wa pili kutoka kulia) akifafanua jambo wakati wa ukaguzi wa bwalo la wanafunzi. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Wizara ya Nishati na Madini, Caroline Musika akifuatiwa na Mkuu wa Kitengo chaTehama, Wizara ya Nishati na Madini, Francis Fungameza. Wa kwanza kulia ni Mshauri Mwelekezi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya PSM Architects Ltd, Peter Matinde.
 Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Wizara ya Nishati na Madini, Caroline Musika akikabidhiwa funguo za jengo la hosteli la Chuo cha MRI na Mkandarasi  aliyejenga jengo hilo kutoka kampuni ya Chichi Engineering Construction Ltd, Shaibu Katindi. Wanaoshuhudia ni Msanifu Majengo wa SMMRP, Arch. Joseph Ringo (kulia), Mkuu wa Chuo cha MRI, Mhandisi Oforo Ngowi (kushoto kwa Mkandarasi), Maafisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini na washauri waliosimamia ujenzi wa jengo hilo. 
 Mkuu wa Chuo cha Madini cha Dodoma, Mhandisi Oforo Ngowi (wa pili kutoka kulia) akifafanua jambo wakati wa ukaguzi wa bwalo la wanafunzi. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Wizara ya Nishati na Madini, Caroline Musika akifuatiwa na Mkuu wa Kitengo chaTehama, Wizara ya Nishati na Madini, Francis Fungameza. Wa kwanza kulia ni Mshauri Mwelekezi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya PSM Architects Ltd, Peter Matinde.
 Mkandarasi kutoka kampuni ya Chichi Engineering Construction Ltd, Shaibu Katindi (kulia) akielezea jambo kabla ya kuanza kwa ukaguzi wa jengo la hosteli. Wengine katika picha ni wakaguzi pamoja na washauri waliosimamia ujenzi wa jengo hilo.
 Msanifu Majengo wa SMMRP, Joseph Ringo (mwenye shati jeupe) akifafanua jambo katika kikao na Mkuu wa Chuo cha Madini cha Dodoma, Mhandisi Oforo Ngowi (mbele katikati) mara baada ya kuwasili chuoni hapo. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Tehama, Wizara ya Nishati na Madini, Francis Fungameza na kushoto kwake ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Nishati na Madini, Caroline Musika.

 Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Wizara ya Nishati na Madini, Caroline Musika (kulia) akiwa sambamba na Wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mkandarasi pamoja na baadhi ya washauri waliosimamia ujenzi wakimsikiliza Mshauri Mwelekezi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya PSM Architects Ltd, Peter Matinde (hayupo pichani) wakati wa ukaguzi wa jengo la hosteli.

 Mshauri Mwelekezi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya PSM Architects Ltd, Peter Matinde (kulia) akielezea jambo mara baada ya kufanyika kwa ukaguzi wa jengo la hosteli la MRI. Sambamba nae ni Wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini na  Mkandarasi.
 Moja ya chumba cha jengo lililokabidhiwa la hosteli ya wasichana ya Chuo cha Madini (MRI) Dodoma. 
 Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Wizara ya Nishati na Madini, Caroline Musika (kushoto) akiendelea na ukaguzi katika moja ya chumba katika jengo la hosteli. Katikati ni Mkuu wa Kitengo cha Tehama, Wizara ya Nishati na Madini, Francis Fungameza.
 Bwalo la wanafunzi wa Chuo cha Madini Dodoma baada ya kukarabatiwa na kupanuliwa.


JENGO LA HOSTELI CHUO CHA MADINI LAKAMILIKA

Wizara ya Nishati na Madini imepokea jengo la hosteli ya wasichana ya Chuo cha Madini cha Dodoma (MRI) kutoka kwa Mkandarasi wa Kampuni ya Chichi Engineering Construction Limited katika makabidhiano yaliyofanywa hivi karibuni, mkoani Dodoma mara baada ya ujenzi kukamilika.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja Mradi wa  Usimamizi  Endelevu wa  Rasilimali Madini (SMMRP), Mhandisi Idrisa Yahya, wakati wa makabidhiano hayo Msanifu Majengo (Architect) wa SMMRP, Joseph Ringo alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kutapunguza uhaba wa nafasi za malazi kwa wanafunzi hususan wa kike katika chuo hicho.

Aidha, alisema kulingana na takwimu za MRI inaonyesha kila mwaka usaili wa wanafunzi unaongezeka na kwa kuwa chuo hicho hakina hosteli za kutosha, inawalazimu wanafunzi wengi kupanga vyumba nje ya chuo jambo ambalo alisema si jema kwa wanafunzi hao.
“Kila mwaka wanafunzi wanaongezeka, kwahiyo kupitia jengo hili jipya la hosteli ya wasichana nina imani changamoto ya malazi kwao itakuwa imetatuliwa,” alisema.

Katika makabidhiano hayo, ilielezwa kuwa jengo hilo la hosteli linao uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 88.Aidha, mbali na jengo hilo la hosteli, makabidhiano hayo pia yalihusisha bwalo la wanafunzi ambalo likikuwa limekarabatiwa kwa kupanulia pamoja na ofisi ya Mkuu wa Chuo.

Ringo alieleza kuwa, makabidhiano hayo yanakamilisha Awamu ya Kwanza ya Mradi wa SMMRP kwa chuo hicho na kuongeza kuwa matarajio ya baadaye ni kujenga miundombinu zaidi ili kukidhi mahitaji ya chuo hicho.“Mahitaji ya chuo kuhusiana na majengo ni makubwa kuliko haya yaliyojengwa,” alisema.

Akizungumzia mikakati ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya mradi wa SMMRP (Additional Financing), Msanifu Ringo alisema hatua zote za kuanza utekelezaji zimeanza.

“Matarajio yetu ni kuwa malengo yaliyopangwa yatafikiwa kwa muda uliopangwa. Mradi huu umebeba dhima kubwa ya kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi na sekta  ya Madini," alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho cha Madini, Mhandisi Oforo Ngowi, alisema mradi huo wa ukarabati na ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Chuo, bwalo la wanafunzi na hosteli unao umuhimu wa kipekee katika kuboresha miundombinu pamoja na kuleta maendeleo endelevu ya chuo hicho.

“Huu ni ukombozi mkubwa sana kwa wanafunzi waliokuwa wanahangaika kutafuta malazi nje ya chuo. Kilichobaki hapa ni kusoma tu”, alisema.
Mradi huo wa Chuo cha Madini uliokabidhiwa umefadhiliwa na Benki ya Dunia chini ya usimamizi wa SMMRP na ulianza Julai, 2014 na kukamilika mwaka huu 2016 na ilielezwa kwamba umegharimu takriban milioni 997.

Aidha jengo hilo la hosteli limebuniwa na kampuni ya ubunifu Majengo ya PSM Architects Ltd kwa kushirikiana na Howard Humphreys (T) Ltd na Mas-Q Associates Ltd.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotekeleza miradi mbalimbali ya sekta ya madini chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.


No comments: