Saturday, February 20, 2016

DK KALEMANI AIKATAA RIPOTI YA MENEJA TANESCO BUHIGWE

Mkuu wa Wilaya mpya ya Buhigwe, Mary Tesha akiwasilisha taarifa kuhusu kero na changamoto mbalimbali kuhusu sekta ya nishati, zinazowakabili wananchi wake mbele ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani (wa pili kutoka kulia), alipofanya ziara wilayani humo hivi karibuni.

Na Veronica Simba - Buhigwe

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani amekataa kupokea Taarifa ya utendaji kazi kwa Wilaya mpya ya Buhigwe mkoani Kigoma, kutoka kwa Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wa Wilaya hiyo, Ntungwa Njegelo. Dk Kalemani alikataa kupokea taarifa hiyo juzi Februari 19, alipokutana na Uongozi wa Wilaya hiyo mpya, kwenye Ofisi ya muda iliyopo wilayani humo, akiwa pamoja na watendaji mbalimbali kutoka wizarani, Tanesco na Wakala wa Umeme Vijijini (REA)

Akizungumzia sababu za kukataa kupokea taarifa hiyo, Naibu Waziri alisema haijitoshelezi kwani haijaeleza kwa kina masuala mbalimbali muhimu ya kiutendaji katika wilaya hiyo.


“Kwa mfano, taarifa hii inaeleza vijiji 12 vimepata umeme lakini haielezi idadi hiyo ni kati ya vijiji vingapi. Pia, haielezi ni asilimia ngapi ya umeme imepatikana. Taarifa hii haiwezi kunisaidia maana nataka kutatua kero hivyo ni lazima nijue ukubwa wa tatizo.”
Kufuatia hatua hiyo, Naibu Waziri Kalemani alimwagiza Meneja huyo aandae taarifa mpya, yenye maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme hususani mradi wa REA (Umeme Vijijini) Awamu ya pili na kuiwasilisha kwake Jumatatu, Februari 22 mwaka huu.

Aidha, Dk Kalemani alimwagiza Meneja huyo kufuatilia na kufanyia kazi malalamiko ya wananchi katika eneo lake, kuhusu kuwepo na mashimo yaliyochimbwa kwa ajili ya kusimika nguzo za umeme katika mashamba yao lakini yameachwa wazi kwa muda mrefu pasipo zoezi hilo kufanyika hivyo kuwazuia kuendelea na shughuli zao za kilimo.

Awali, akiwasilisha taarifa kwa niaba ya wananchi wake kuhusu kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili kuhusiana na sekta ya nishati, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mary Tesha alimwomba Naibu Waziri kusaidia ili mashimo yaliyochimbwa katika baadhi ya vijiji kwa ahadi ya kusimika nguzo za umeme, yafanyiwe kazi mapema ili wananchi waendelee na shughuli za kilimo katika mashamba yao.

Vilevile, Dk Kalemani alisema pamoja na mapungufu kadhaa, Tanesco wamejitahidi kufanya kazi nzuri ya kuwaunganishia wananchi wa vijijini umeme kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Alimpongeza Mkandarasi mzalendo anayeunganisha umeme wa REA Awamu ya pili mkoani Kigoma, Wilbroad Mutabuzi kupitia kampuni yake ya JV State Grid Electrical and Trchnical Works Ltd kwa kazi nzuri anayoifanya.

“Kuna baadhi ya maeneo tumekutana na matatizo ya wakandarasi kufanya kazi chini ya kiwango hivyo kuturudisha nyuma. Huyu Mkandarazi mzawa anayefanya kazi hiyo hapa Kigoma anajitahidi sana na namtaka aendelee hivyo.”

Alisema ameagiza zoezi la kuunganisha umeme wa REA Awamu ya pili likamilike ifikapo Mwezi Aprili mwishoni, hivyo wale wote waliopangwa kuunganishiwa umeme katika awamu hiyo, wanapaswa kuwa wamepatiwa huduma hiyo ndani wa kipindi hicho.

Naibu Waziri Kalemani yupo katika ziara ya kikazi kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya wizara yake. Alianza ziara hiyo mkoani Tabora, sasa yupo Kigoma na anatarajia kumalizia ziara hiyo ya siku 10 mkoani Geita.

1 comment:

Anonymous said...

Hapa Kazi tu
Hawa jamaa wa magufuli si mchezo.