Friday, January 1, 2016

WAZIRI PROF. MBARAWA AWATAKA TAA NA TCAA KUBORESHA HUDUMA NA KUONGEZA MAPATO

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akipata maelezo ya uboreshaji unaoendelea kufanyika wa kiwanja cha Ndege Terminal Two kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Eng. Suleiman Suleiman jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa TAA Eng. Suleiman Suleiman akimwonyesha Waziri Prof. Mbarawa ujenzi unaoendelea wa jengo la tatu la abiria (Terminal three), ambapo jengo hilo likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 6 kwa mwaka.
Mkurugenzi wa TAA Eng. Suleiman Suleiman akimwonyesha Prof. Makame Mbarawa eneo ambalo limefanyiwa ukarabati kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere International Airport (JNIA), wakati alipotembelea eneo hilo, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiongea na wafanyakazi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA), na kuagiza Mamlaka hiyo kuongeza mapato ili kuweza kupanua fursa za uwekezaji na kuendeleza uchumi wa nchi.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametembelea Mamlaka ya Viwanja  vya ndege (TAA) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA) jijini Dar es salaam na kuagiza Mamlaka hizo kuboresha huduma na kuongeza mapato ili kupanua fursa za uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi.

Waziri Mbarawa amesisitiza kuwa mapato yatakayokusanywa yawe yanatoka kwa makampuni ambayo yapo chini ya mamlaka hizo na si kwa kuwabana wananchi.

‘Nataka msiongeze mapato kwa kuwaathiri wananchi na badala yake  mtafute vyanzo vingine vya mapato ambavyo vitasaidia katika kuchochea fursa za uwekezaji’, amesema Waziri Mbarawa.

Aidha, Profesa Mbarawa ametaka huduma zote katika viwanja vya ndege kama zima moto,uhamiaji,polisi na huduma za afya, ziwe chini ya mamlaka ya viwanja vya ndege  ili kurahisisha uharaka na ukaribu wa huduma kumfikia mteja kwa urahisi.

‘Ninyi ndio kioo cha jamii, hivyo basi haipaswi kuchukua zaidi ya dakika kumi kumhudumia mteja mmoja au kuwa na tabia ya kumsumbua mteja pindi anapohitaji huduma’, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Ameitaka TAA kufanya utaratibu wa kujenga jengo kubwa la ofisi kwa ajili yao na kukodisha kwani kufanya hivyo kutaongeza mapato katika Mamlaka hiyo.

Awali wakati akitoa taarifa kwa Waziri Mbarawa Mkurugenzi wa TAA Eng. Suleiman Suleiman amesema kuwa Mamlaka hiyo imeweza kuhakikisha kuwa huduma za usafirishaji  kama za ufundi na zimamoto na uokoaji zinaridhisha.

Katika hatua nyingine wakati akiwa katika Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa uharaka katika uendaji kazi wao ili kuendana na kasi ya mabadiliko anayoitaka Rais John Pombe Magufuli

“Najua ni waadilifu katika kazi zenu ila nawaomba muongeze, pasiwe na usumbufu kila mtu ana haki ya kupata huduma stahiki anayohitaji na kwa wakati unaotakiwa” amesisitiza Waziri Mbarawa.

Ameitaka TCAA kujitathmini wao binafsi, wateja na huduma wanazozitoa kwa wateja wao ili kuhakikisha sekta yao inakuwa. 

Naye Kaimu Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Charles Chacha ameitaja baadhi ya miradi inayotekelezwa na Mamlaka hiyo kuwa ni uwekaji wa mitambo ya kisasa ya kuongoezea ndege na kufuatilia safari za ndege nchini iitwayo ‘Automatic Dependent Surveillance’. 

Ameainisha kuwa mradi mwingine ni ununuzi wa rada mbili za kuongozea ndege za kiraia ambazo zitafungwa katika viwanja vya Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es salaam na KIA mkoani Kilimanjaro.

IMETOLEWA NA 
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO 
WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO.

No comments: