Friday, January 15, 2016

MAELEZO YA WAZIRI KUHUSU TIBA ASILI NA TIBA MBADALA

 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO

Ndugu Wananchi,
Katika nchi yoyote ile uhuru usio na mipaka ni jambo la hatari; lakini pia hakuna haki isiyo na wajibu. Vivyo hivyo, katika huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala hapa nchini kuna Sheria, Kanuni na Taratibu za Maadili zinazoweka masharti, uhuru na mipaka; pia haki na wajibu wa kila mdau. Huduma za tiba asili na tiba mbadala ni huduma zinazotambulika na Jamhuri yetu, watu wake na ina thamani kubwa. Aidha, ni huduma inayotambuliwa na sayansi ya tiba ya kisasa. Hata hivyo huduma hizo zimekumbwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa watoa huduma wasiozingatia Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali. Kutokana na hali hiyo na kutokana na ziara ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Hamisi A. Kigwangalla (Mb) kwa Tabibu Juma Mwaka Juma tarehe 14/12/2015 na kufuatia uchambuzi uliofanywa na Wizara baada ya ziara hii, Wizara imebaini changamoto zifuatazo:-
1.   Huduma za tiba asili na au tiba mbadala zinatolewa na watoa huduma wasiosajiliwa na Mamlaka husika kwa mujibu wa Sheria.
2.   Uwepo wa vituo vinavyotoa huduma za Tiba Asili na au Tiba Mbadala bila kusajiliwa kwa mujibu wa Sheria.
3.   Kutolewa dawa kwa wagonjwa bila dawa hizo kusajiliwa na mamlaka husika.
4.   Uingizaji na matumizi ya vifaa vya uchunguzi ambavyo havijasajiliwa na mamlaka zinazohusika, na
5.   Utoaji wa matangazo bila ya kufuatwa kwa matakwa ya sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo. Aidha baadhi ya matangazo hayo yamekuwa na taarifa zinazoweza kuleta madhara na kupotosha Umma wa Watanzania.

Ndugu Wananchi,
Kutokana na hali hiyo, Wizara itahakikisha kuwa huduma za tiba asili na tiba mbadala zinatolewa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo. Lengo ni kuwezesha huduma za tiba asili na tiba mbadala zinakuwa huduma rafiki na salama kwa watumiaji. Tunao wajibu wa kuwalinda wananchi, vile vile tunaowajibu wa kuweka mazingira mazuri kwa watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala ili kufanya shughuli zao vizuri.  

Hivyo kwa upande wetu Wizara itahakikisha kuwa:-
1.   Baraza na sehemu inayosimamia huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala inakuwa na watumishi wa kutosha kwa mujibu wa Ikama.
2.   Kunakuwa na Mpango Mkakati wa muda mrefu kuwezesha kufanikisha uboreshaji wa huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini.
3.   Watoa huduma wote, vituo vyote vya kutolea huduma, dawa na vifaa na vifaa tiba vinavyotumika vinasajiliwa.
4.   Utaandaliwa mwongozo wa mafunzo kwa watoa huduma wote nchini, kuhusu namna ya kuweka kumbukumbu za wagonjwa, kutoa rufaa kwa wagonjwa na kutengeneza dawa zilizo bora.
5.   Kunakuwa na mawasiliano na Wizara zinazohusika na habari na mawasiliano ili kuboresha utoaji matangazo yanayohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala.
6.   Kunakuwa na mawasiliano na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Taasisi za Utafiti ili kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini.
7.   Tutafanya mabadiliko ya Sheria ili kuongeza kiwango cha adhabu kwa watakaokiuka, na pia tunakusudia kuondoa Kanuni inayoruhusu matangazo kwa idhini ya Baraza kwa sababu inaweka mianya ya matumizi mabaya ya fursa ndogo ya matangazo inayotolewa.

Ndugu Wananchi,
Katika kufanikisha hayo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatoa maelekezo yafuatayo kwa watoa huduma na jamii:-
1.    Hairuhusiwi kwa mtu yeyote kutoa huduma za tiba asili na au tiba mbadala bila kusajiliwa. Ninalielekeza Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kuhakikisha kuwa watoaji huduma wote wanasajiliwa kwa mujibu wa Sheria:
(a)  Mijini, (Majiji, Manispaa na Miji) - usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi mitatu; kuanzia Januari 15, 2016 na
(b) Vijijini, Halmashauri zote zilizobaki - usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi sita kuanzia Januari 15, 2016.
Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakaye puuza kujisajili katika kipindi hicho
2.   Hairuhusiwi kuuza na au kugawa dawa yoyote ile ya tiba asili au tiba mbadala mpaka iwe imesajiliwa na Baraza baada ya kuchunguzwa na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa ni salama na kupewa kibali na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
3.   Hairuhusiwi kuendesha kituo cha kutolea huduma za tiba asili na au tiba mbadala bila kukisajili.
4.   Wizara inapiga marufuku kwa mtu binafsi au taasisi yoyote ile kutumia kifaa au kifaa tiba chochote bila kukisajili TFDA na kupewa kibali; na
5.   Matangazo yote yanayohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala ambayo hayajapitishwa na Baraza yamezuiliwa kuanzia leo tarehe 15/1/2016. Wizara inavitaka vyombo vya Habari hasa Televisheni, Radio na Magazeti kuzingatia Sheria na Kanuni za Tiba Asili na Tiba Mbadala inayozuia matangazo ambayo hayajachunguzwa na Baraza. Ni wajibu wa vyombo vya habari  kujiridhisha na Mamlaka husika yaani Baraza kabla ya kutoa tangazo lolote linalohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala. Wizara itashirikiana na Mamlaka zinazohusika  na habari na mawasiliano kutekeleza agizo hili. Vile vile, hairuhusiwi kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara kuhusu tiba asili na tiba mbadala.

Ndugu Wananchi,
Katika kuwezesha ulinzi wa afya za wananchi, kila mmoja wote alinde afya yake kwa kuhakikisha kuwa huduma anayopata ya tiba asili na tiba mbadala ni kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Miongozo inayotolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Ni uhakika uliowazi kuwa kwa pamoja tukiboresha huduma za tiba asili siyo tu tutaboresha afya zetu bali pia tutaweza kuuza dawa na huduma hizo nje ya nchi na kupata fedha za kigeni kupitia na hivyo kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja, jamii na nchi kwa ujumla. 
Kwa pamoja tushirikiane kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini. Inawezekana. 

Ummy A. Mwalimu (Mb)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO

15 Januari, 2016

1 comment:

Anonymous said...

The mdudu, Asante sana MAMA kumbe mnayaweza tuna wapenda na tupo nyuma yenu kina Mama zetu na Madada zetu SHOKA kama nyie maana nyie ndio tunao wategemea coz mkicheza na maisha yetu sote twafa so tulindeni kama hivyo.