Wednesday, November 25, 2015

Serikali yawataka wachambuaji na wasambazaji wa mbegu za pamba kuacha kuwasambazia wakulima mbegu zilizozalishwa kwenye maeneo yenye ugonjwa wa mnyauko fusari

Serikali imewataka wachambuaji na wasambazaji  wa mbegu za pamba kuacha kuwasambazia wakulima mbegu zilizozalishwa katika maeneo yaliyobainika kuwa na ugonjwa wa mnyauko fusari (Fusarium Wilt Disease).  Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi, Bodi ya Pamba Tanzania, Bwana James Shimbe.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Bwana Shimbe amesema, ugonjwa wa mnyauko fusari unaweza kudhibitiwa ikiwa wakulima wa pamba watatumia mbegu bora kutoka kwa wasambazaji wanaotambulika na Bodi ya Pamba Tanzania.

Akizungumzia tatizo la kuenea kwa ugonjwa huo Bwana Shimbe amesema kwa kiasi fulani limetokana na baadhi ya wachambuaji wasio waaminifu kuendelea kusambaza mbegu za pamba za kupanda ambazo zinaweza kuwa zimetoka katika maeneo yaliyobainika kuwa na  ugonjwa wa mnyauko fusari.

“Tulishatoa maelekezo kwa kuwataka wasambazaji wa mbegu za pamba za kupanda kutosambaza mbegu zilizozalishwa katika maeneo yenye ugonjwa.”

Hivyo tunaendelea kusisitiza kuwa wakulima wawe makini wanapo nunua mbegu kutoka kwa wasambazaji wasiotambulika na watoe taarifa haraka kwa Bodi wanapoona mbegu hizo hazioti ili hatua za haraka zichukuliwe za kupeleka mbegu zingine mbadala ili kuendana na msimu wa kilimo.

Aidha, Bwana Shimbe amewataka wachambuaji wa pamba ambao ndio wasambazaji wa mbegu kuacha mara moja kuwasambazia wakulima mbegu ambazo zimetoka kwenye maeneo yaliyobainika kuwa na ugonjwa na badala yake mbegu za pamba hizo zisindikwe kuzalisha mafuta ya kula kama walivyokuwa wameelekezwa na Bodi hapo awali.

“ Bodi ilishatoa maelekezo kwa wachambuaji wote wa pamba kote nchini,  kutenga mbegu za pamba za kupanda  msimu huu wa kilimo kutoka maeneo yaliyo salama kwa kuziwekea lebo ili  kuzitofautisha na zile zinazotoka kwenye maeneo yaliyobainika  kuwa na ugonjwa, ambapo  zile zinazotoka katika maeneo yenye ugonjwa zisitumike kama mbegu za kupanda, bali zisindikwe kupata mafuta ya kula kama sehemu ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa, na zile mbegu ambazo zimetoka kwenye maeneo yasiyo na ugonjwa zisambazwe kwa wakulima kwa ajili ya kupanda kwenye mashamba yao baada ya kufanyiwa majaribio ya uotaji (seed germination test) na taasisi inayohusika na udhibiti wa ubora wa mbegu (TOSCI)”

 Aidha, mbegu zinazofaa kutumika kwa sasa ni UKM08 iliyofanyiwa utafiti na Kituo chetu cha Utafiti cha Ukiriguru, ambayo ubora wake umethibitishwa na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) na inauwezo wa kuhimili magonjwa pamoja na uzalishaji wenye tija zaidi. Mbegu hiyo itakuwa inaiondoa kwenye uzalishaji ile ya zamani  ya UK 91 ambayo imepungua ubora wake. Katika msimu huu wa kilimo wa 2015/16 Mbegu ya UKM08 itaendelea kuzalishwa kwa wingi (seed multiplication) katika maeneo salama yasiyo na ugojwa wa mnyauko fusari katika mkoa wote wa Singida na wilaya ya Nzega na Igunga, mkoa wa Tabora.

Bwana Shimbe ametoa wito kwa wakulima na wadau wote wa pamba nchini kufuata kanuni za kilimo bora cha pamba ikiwa ni pamoja na kutumia mbegu bora za pamba.  Aidha, baadhi ya mawakala wa ununuzi wa pamba mbegu na wakulima wenye tabia ya kuchanganya pamba mbegu na maji, mchanga, chumvi na kemikali zingine kama vile “mafuta ya kenge” kwa madai ya kuongeza uzito kwenye pamba yao waachane na tabia hiyo potofu, kwani kwa kufanya hivyo kunachangia kuoza kwa kiini cha mbegu na kuharibu ubora wake na hivyo kusababisha mbegu kutokuota.

Imetolewa:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika
Kilimo Complex
1 Mtaa wa Kilimo 15471
DAR ES SALAAM

No comments: