Thursday, July 2, 2015

MAKALA YA MDAU KUTOKA UKEREWE-KINANA AMENIKUMBUSHA HOTUBA YA MWALIMU NYERERE

NA HAFIDH KIDO, Ukerewe

MWAKA 1995 kulikuwa na vuguvugu la vyama ya siasa kurithi kiti cha Rais wa awamu ya pili Ally Hassan Mwinyi, hasa ikizingatiwa ulikuwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi. Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichoshika dola pamoja na vyama vya upinzani kama NCCR-Mageuzi ya Augustino Lyatonga Mrema na Chama cha Wananchi (CUF), ni nani mwenye sifa ya kuongoza Tanzania.

Mambo yalikuwa mengi lakini udini na ukabila vilishika nafasi kubwa, Rais wa Kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere kwa kuwa wakati huo alikuwa mzee pekee aliyezungumza na Tanzania nzima pamoja na nchi jirani wakakaa kimya kumsikiliza, hivyo aliamua kuzungumza alipokutana na waandishi wa habari katika Hoteli ya Kilimanjaro.

Alisema mengi lakini lililobaki katika vichwa vya wengi nikiwemo mimi ni kuhusu sifa za rais aliyetakiwa wakati huo, Mwalimu alisema “Utakuta mtu anasema huyu sifa zooote anazo lakini mhh Mkara, ndio Mkara…” Jumatatu wiki hii nilibahatika kutembelea visiwa vya Ukerewe mkoani Mwanza, miongoni mwa visiwa nilivyotembelea ni Irugwa na Ukara halafu nikamalizia Ukerewe katika Kata ya Nansio nilipopitisha usiku.

Nilipofika Ukara mwangwi wa hotuba ya Mwalimu Nyerere ulinijia kuwa yeyote anaweza kuwa rais wa nchi, vigezo vya kuwa mtu wa hali ya chini au kutoka katika eneo duni na ukoo usiotajika haliangaliwi na wananchi.
Nimezunguka na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana katika mikoa tisa ya nchi hii, katika hiyo tisa nimezunguka wilaya na majimbo yote ya uchaguzi. Malalamiko makubwa waliyokuwa nayo wananchi ni maji, umeme na ardhi. Wabunge na Mawaziri hawafiki kwa wananchi kusikiliza matatizo yao.

Kila tulipopita malalamiko yaliyokuwepo huwezi kuamini kuwa eneo hilo lina kiongozi, serikali ina utaratibu wa namna mbili za kuongoza nchi kubwa namna hii; kwanza kuna mwakilishi nwa serikali kuu, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Mkoa na Wilaya (DAS na RAS).Halafu kuna mwakilishi wa serikali za mitaa, Mbunge, Diwani, Meya, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa na Mwenyekiti wa Kijiji.

Wte hao hawahangaiki kutatua matatizo ya wananchi wanasubiri mwaka wa uchaguzi ufike washughulikiane, mara nyingine wanapokutana katika vikao vya maamuzi kama baraza la madiwani na kikao cha Bunge, hakuna kinachofanyika zaidi ya kuonyeshana chama gani kina msemaji mzuri.

Wabunge wa CCM, ambao wanaaminika kwa kupewa dhamana ya kuongoza serikali nao wanaingia katika mkumbo wa kukubali kila kitu kinachotakiwa na serikali bila kujali jimboni suala hilo litapokelewa vipi.
Nikilinganisha na mbio za urais mwaka huu naona kila mmoja anajipigia debe kutokana na fedha alizonazo, maana yake wakati wananchi watakapopewa ridhaa ya kuchagua hapoa Oktoba 25, 2015 wapo watakaosema mgombea huyu sifa zote za urais anazo lakini masikini, au Mwislamu/Mkristo.

Kwa kiasi kikubwa Tanzania imepiga hatua katika kukomesha ukabila, lakini dhambi ya udini na hongo bado havijapatiwa tiba. Ni saratani inayowatafuna wapiga kura kwa kipindi kirefu tangu kurudi mfumo wa vyama vingi.
Mtu atakayepata bahati ya kuisikiliza, kuisoma au kuitazama hotuba ile kwa mara nyingine atabaini kuna mambo mengi yanajirudia.Masuala ya ukabila na udini hayana maana wala nafasi katika Tanzania ya sasa, uwe Mkara, Mmwera, Mdigo au Msomali wananchi wanachotaka ni utendaji wako.

Nitatoa mfano, niliwasili namsafara wa Kinana katika kisiwa cha Irugwa saa nane mchana, tulitoka Mwanza usiku saa sita maana yake tulikaa ndani ya maji ya Ziwa Victoria kwa saa 13 tukiwa na Kivuko FB Chacha.
Wenyeji walituambia tungetumia boti za mashine tungetumia saa atu mpaka nne, lakini kwa kuwa msafara ulitaka kwenda na magari ilitulazimu kutumia kivuko kinachokwenda taratibu.Nilipofika Irugwa nilizungumza na Mzee Salvatory Mang’ula (67), aliniambia kisiwa hicho mbali ya kuwa na zahanati na shule mbili lakini hakuna gari hata moja.

“Hapa kulikuwa na gari moja tu aina ya Land Rover la Namrasa ni daktari alisomea huko mjini akaja na gari mwishoni mwa miaka ya 1990, lakini liliharibika mwaka 2003 na huo ukawa mwaka wa mwisho kushuhudia gari katika kisiwa chetu,” alisema Mzee Mang’ula. Tafsiri yake ni kuwa watoto waliozaliwa mwaka 2004 na kukosa bahati ya kutoka nje ya kisiwa hicho watakuwa hawajasikia mlio wa gari hadi wanafikisha umri wa miaka 11.

Tuachane na hayo, Mzee Mng’ula aliniambia, “Tunapotaka kwenda visiwa vya jirani kama Ukerewe, Ukara na vingine vidogo inatulazimu kupitia kisiwa cha Majita kilicho Mkoa wa Mara halafu tunarudi wilayani Ukerewe.
“Mbunge wetu hana lolote alilolifanya, ahadi alizotoa mara ya mwisho alipokuja kushukuru baada ya kumchagua pia hakuitimiza. Mimi kila siku ninamuona kwenye luninga tu akiwa bungeni, lakini haji hapa na si yeye tu hata viongozi wengine hawaji, huyu Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe hajakanyaga ndio ninamuona leo kwenye ziara ya Kinana.

“Hakuna kiongozi wa kitaifa aliyewahi kukanyaga kisiwa hiki tangu nilipozaliwa mwaka 1946, huyu (Kinana) ndiye kiongozi pekee wa kitaifa kufika hapa, mara ya mwishi mwaka 1976 alikuja Mkuu wa Mkoa wa Ziwa Magharibi, Lawi Nangwanda Sijaona wakati huo akiwa Mkuu wa Mkoa huu.” Kwa kifupi inaonyesha ni namna gani viongozi wa serikali hawatilii maanani shida za wananchi, watu kama hawa ikiwa mbunge wao hana habari nao serikali itafanya nini, wanakumbukwa kipindi cha uchaguzi tu upepo ukishapita kwisha habari yao.

Kinachonifurahisha ni namna Kinana anavyoshughulikia matatizo kama hayo, hapohapo alipokuwa visiwani alipiga simu kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Muijage akaahidi kupeleka umeme wa jua visiwani humo kwa sababu gridi ya taifa haikuwapitia, hata ule umeme wa mradi wa umeme vijijini (REA) umewakosa.
Niliingia kisiwa cha Ukara saa 12 jioni, ni mji uliochangamka una watu wengi na shughuli za uvuvi ndizo zinazowapatia kipato. Huduma muhimu kama umeme na maji bado tatizo, kinachinishangaza visiwa hivyon vinalalamikia maji safi ya kunywa huku vimezungukwa na ziwa kubwa lililounganisha nchi tatu za Afrika Mashariki, viongozi wamelala usingizi wa pono.

Hivyo, kaulimbiu yangu mwaka huu wananchi wawe makini katika kuchagua, usimchague mtu kwa sababu ni ndugu yako au amekununua, wala usiache kumchagua mtu kwa sababu unamchukia kabila au dini yake, angalia uwezo.

Mwalimu Nyerere katika hotuba hiyohiyo aliweka kichombezo kuwa Watanzania hawaangalii dini kwa sababu hawataki Padri wala Sheikh wa kuwasalisha bali wanataka mtu atakayeangalia maslahi ya nchi yao.
Kila alipopita Kinana aliacha ahadi ya kutekelezeka, na aliposhindwa alitafuta namna ya kumpigia Rais Jakaya Kikwete au waziri mwenye dhamana ya suala linalojadiliwa iwe ardhi, maji au umeme.

Kilichonishangaza ni kuwa hata waziri mwenye dhamana ya maliasili na utalii ajawahi kukanyaga ardhi ya visiwa hivyo, visiwa vyenye hazina kubwa ikiwa vitatumiwa vizuri kwa maslahi ya uchumi wa nchi.
Viongozi waache kunogewa na viyoyozi ofisini, waunde kikosi kazi kitakachozunguka kusikiliza matatizo ya wananchi; nchi hii ni kubwa wasiamini kuwa kukaa Dar es Salaam na Dodoma kila kitu kimekamilika, kuna kazi yakuimaliza Tanzania na watu wapo wanajua kila kitu siku hizi mitandao ya kijamii inahabarisha wengi.

No comments: