Friday, May 22, 2015

HAKUNA MAENDELEO BILA NISHATI ENDELEVU - KITWANGA

Mhe. Charles Kitwanga ( Mb) Naibu Waziri, Nishati na Madini akizungumzia namna Tanzania inavyotekeleza Mkakati wa Nishati Endelevu kwa Wote (SE4All) wakati wa Mkutano wa siku Mbili wa Mawaziri wa Sekta ya Nishani, uliofanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini ambao wamefuatana na Naibu Waziri katika mkutano huu muhimu uliojadili kwa kina nafasi na umuhimu wa nishati endelevu kwa wote katika kusukuma mbele malengo ya maendeleo endelevu , ukuaji wa uchumi, maendeleo ya jamii na utunzaji wa mazingira.
Mhe. Kitwanga akiteta jambo na Mwakilishi wa Bank ya Maendeleo kwaajili ya Afrika AfDB muda mfupi mara baada ya Naibu Waziri kuzungumza , mkutano huu wa SE4All, pamoja na Mawaziri wa sekta husika umewashirikisha pia wadau mbalimbali wakiwamo wakuu wa vyombo vya fedha kama vile Bank ya Dunia, AfDB na wataalamu wengine wakiwamo pia wanamziki maarufu ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakichagiza na kuwekeza katika nishati endelevu.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Ngosi Mwihava akiwasilisha Action Agenda of Tanzania kuhusu SE4All katika moja ya mikutano iliyofanyika hapa jijini New York.
Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Ngosi Mwihava akiwa na wataalamu wake na wataalamu washauri wakibadilishana mawazo kuhusu Action Plan of Tanzania.

Na  Mwandishi Maalum,  New York

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  inaamini kwamba,   utekelezaji wa   mipango  na  malengo ya  mbalimbali  ya maendeleo  hayataweza kupatika  au kufikiwa kwa haraka  pasi na uwepo wa nishati endelevu na kwa wote.

Ni kutokana na kulitambua hilo,   Tanzania  imejikita  kikamilifu katika kukuza  uwezeshaji wa  matumizi ya teknolojia za kisasa na mbinu za kuongeza  upatikanaji wa  huduma  za kisasa za nishati ikiwa ni pamoja na kuongeza maradufu kiwango cha uboreshaji na ufanisi wa nishati mbadala  ili kuchagiza maendeleo.

Hayo yameelezwa siku ya Alhamisi na Naibu   Waziri wa Nishati na  Madini, Mhe. Charles Kitwanga ( Mb), wakati  akizungumza katika siku ya pili ya   majadiliano ya mawaziri wanaohusika na   sekta ya nishati ambapo  kila  waziri aliyehudhuria mkutano huo  alipata fura ya kuelezea    na kutoa ahadi  ya namna inavyotekeleza mkakati wa  nishati endelevu wa wote (SE4All).

Mhe. Kitwanga na ujumbe wake unaowashirikisha wataalamu mbalimbali kutoka  Wizara ya Nishati na Madini akiwano   Kaimu   Katibu  Mkuu, Bw.  Ngosi Mwihava wameshiriki  kikamilifu katika mkutano huu  ulioitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ambapo tangu  ulipoanza  mapema wiki hii, washiriki wamekuwa wakijadili mada mbali mbali zinazohusiana na  masuala  ya nishati,  uwekezaji  na mchango  wake katika eneo zima la utekelezaji wa  malengo ya maendeleo endelevu.

“ Tanzania   inaamini kwamba  hakuna  ajenda za   maendeleo zinazoweza kufikiwa kwa ukamilifu pasipo   uwepo wa nishati ya uhakika” akasema Naibu Waziri
Na kuongeza kuwa,   mkakati wa  nishati endelevu kwa wote ni nyezo muhimu katika kurahisisha  ukusanyaji na uwekezaji wa raslimali inayohitajika ili kufika malengo  ya  kitaifa ya   nishati endelevu kwa wote kufikia mwaka 2034 kama inayoainishwa katika  mkakati huo.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, Charles Kitwanga,  Tanzania ilipitisha mkakati wa   SE4All  mwaka 2012 na kufuatiwa na  mchakato wa kufanya tathmini  ili kubaini mapungufu ambayo yalipelekea kutoa  taarifa ya tathmini mwaka 2013. 

Baada ya tathmini hiyo ilifuatia  misaada kutoka  SE4All kwaajili ya Afrika iliyosaidia kuandaa rasimu ya Ripoti na  nchi ( Country Action Agenda)  kwa ufadhili wa Banki ya   Maendeleo  ya Afrika, (AfDB) na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ( UNDP).

Kwa mujibu wa Mhe. Kitwanga,  taarifa hiyo inatarajiwa kuwasilishwa kwa  udhibitisho mwezi Agosti, 2015.
Aidha  maandalizi ya Mpango wa Uwezeshaji   umeanza na utalenga katika kuangalia mahitaji ya  haraka ili kuwezesha  mpango huo kuanza kutekelezwa.

Mkutano  kuhusu  Nishati Endelevu kwa wote  (SE4All) umefungwa   jana ( Alhamis).

No comments: