Tuesday, April 28, 2015

Watanzania kunufaika zaidi na Gesi Asilia

Dr Abel Kinyondo & Invited Expert Innocent Bash from TEITI addressing the media  
 Dr Abel Kinyondo Opening Speech . 
 Expert Mr Dennis Rweyemamu (Head - Policy and Research, UONGOZI INSTITUTE) answering questions
 January Makamba and Mujobu Moyo listening to participants
January Makamba answering questions from participants 
Moderator discussing topics with participants 

·       Iwapo kutakuwepo ushirikishwaji wa wananchi
·       Wataalamu nao watoa yao ya moyoni
Na. Mwandishi Wetu
Dar es salaam, Jumatatu Aprili 24, 2015 --KUTOKANA na kugundulika kwa hazina kubwa ya gesi nchini  ambayo inategemewa kukuza pato la taifa zaidi ya mara 15 ya sasa, kiasi cha kuiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati kufikia mwaka 2025.

Hata hivyo, dhana ya kwamba Rais ajaye baada ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake, anaweza akaikuta Tanzania ikiwa ni nchi tajiri tayari kutokana na rasilimali hiyo ya gesi asili, inaweza isiwe sahihi kama hautawekwa mfumo madhubuti wa ushirikishwaji wa wananchi katika fursa zilizopo katika rasilimali hiyo, sera, sheria na usimamiaji mzuri wa raslimali hiyo.

Pia itawezekana tu iwapo viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali hiyo watahakikisha wanaisimamia kikamilifu kwa mujibu wa sera na sheria zitakazotungwa na kusimamiwa na viongozi wenye dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania na nchi yao kwanza.

Hayo pamoja na mengine yalijadiliwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Watanzania wapatao 400 kutoka wilaya mbalimbali ambapo walitoa maoni yao kuhusu ni jinsi gani mapato yatakayotokana na gesi yatawanufaisha wananchi wote wa Tanzania.

Mkutano huo uliowakutanisha Watanzania na kuwawezesha kutoa mawazo na maoni yao kama wawakilishi wa maeneo watokayo uliandaliwa na taasisi za  utafiti kuhusiana na kuondokana na umaskini nchini za REPOA  na Center for Global Development (CGD).

Utafiti huu ni wa kwanza wa aina yake wa kuwashirikisha wananchi wa kawaida katika utafiti unaohusiana na jinsi sera mbalimbali zinatungwa na kutekelezwa kwa matakwa ya matajiri katika nchi zinazoendelea bila kuwaangalia wananchi wa kawaida  wa hali ya chini.

Mtafiti Mwandamizi kutoka taasisi ya CGD, Mujobu Moyo anasema kuwa udhibiti na usimamizi mzuri wa mapato yatakayotokana na gesi yatatoa mustakabali wa nchi yetu utakavyokuwa katika siku zijazo na kuongeza kuwa Tanzania kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazoweza kupelekea gesi iliyogunduliwa isinufaishe wananchi wote.

Moyo alizitaja baadhi ya changamoto hizo, kuwa ni rushwa, ubadhirifu na vurugu za kisiasa.

“Wananchi wanapaswa kwanza kueleweshwa juu ya mchakato mzima na kushirikishwa kutoa maoni yao ni jinsi gani mapato yatakayotokana na raslimali hii yataleta manufaa kwa wote ili kuepuka makosa yaliyojitokeza kwenye nchi nyingine kwa kosa la kutowashirikisha wananchi katika masuala yanayohusu raslimali za Taifa,” Moyo anasema.

Aidha anaeleza kuwa mradi  huu wa utafiti wa CGD, unalenga kufuta dhana iliyozoeleka kuwa Watanzania wa kawaida, kuwa hawana haki ya  kutoa mawazo katika masuala ya kitaifa kama lilivyo suala hili la gesi ambalo limekuwa likijadiliwa na wasomi na wanasiasa.

Moyo anaongeza kuwa ushirikishwaji wa Watanzania wa kawaida, utawawezesha kuelewa suala zima la kugundulika kwa gesi nchini na kupata maoni yao ya jinsi gani ya kusimamia mapato yatakayotokana na gesi kwa manufaa ya wote na hivyo kuongeza uwazi kuhusiana na sula hili.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya REPOA, Prof. Samwel Wangwe, anasema kuongezeka ghafla kwa mapato kutokana na raslimali hizi kunaweza kuleta athari mbalimbali  kwa Tanzania badala ya faida.

Prof. Wangwe, anatoa sababu ya kauli yake hiyo uwezekano wa kuibuka kwa athari mbalimbali kuwa ni pamoja na; kuongezeka kwa vitendo vya rushwa, kuvurugika kwa uchumi, kuongezeka kwa umaskini na kupunguza kukuwa kwa demokrasia.

"Haya yote yanajitokeza iwapo nchi inakuwa na raslimali nyingi na kundi la wananchi wa hali ya chini na wasio na elimu kutopewa taarifa sahihi na za kutosha juu ya kinachoendelea," Prof. Wangwe anatahadharisha.

Akieleza nini kifanyike ili kuondoka na changamoto hizi, Prof. Wangwe anasema: “ Tanzania inaweza kunufaika iwapo itajitayarisha kuingia katika gesi ikiwa imehakikisha kuwa mawazo ya walio wengi yanaingizwa katika utungaji wa sera na hii itasaidia katika mchakato wa wanasiasa kufanya maamuzi na utekelezaji kwa ujumla.”

Mtafiti Mwandamizi kutoka REPOA, Dk. Abel Kinyondo, anasema, “ Kwa zaidi ya miongo minne sasa, Tanzania imeshuhudia ukuaji mzuri wa uchumi licha ya watanzania kuzidi kuwa maskini. Lakini kugundulika kwa hazina kubwa ya gesi nchini kunatoa fursa ya kusahihisha makosa ya nyuma na kubadilisha hali hii.”

Dk. Kinyondo, anaongeza kuwa ili uchumi wa nchi uzidi kukua zaidi kunatakiwa kwanza kujua ni jinsi gani mapato yatakayotokana na raslimali ya mafuta na gesi yatawanufaisha watanzania wote na ndio sababu REPOA na CGD wameamua kuwakutanisha wananchi kutoka sehemu mbalimbali ili watoe mawazo yao kwenye jambo hili muhimu kwa taifa la Tanzania.

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba: "Wananchi wana uwezo wa kuchagua viongozi ambao wanaweza kuweka maslahi yao katika akili na ambao wataweza kusimamia vizuri mapato ambayo yatakayo kuwa yakipatikana kutokana na sekta ya mafuta na gesi."

Mkutano huu ni wa pili katika mwendelezo wa utafiti wa suala hili ambapo mwanzoni wananchi 2,000 kutoka wilaya zote za Tanzania wamehusishwa kutoa maoni yao na wawakilishi 400 waliohudhuria mkutano uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam walipata fursa ya kutoa maoni yao na kupata taarifa mbalimbali kutoka kwa wataalamu.

Utafiti huu unatoa tathmini kuhusu uelewa wa  Watanzania juu ya mchakato mzima wa mafuta na gesi nchini na nini matarajio yao kutokana na raslimali hizi na taarifa za utafiti huu zitasaidia kufanya maamuzi mbalimbali.

Taarifa za mwisho za utafiti huu ziliwasilishwa kwa watungaji wa sera nchini.

Ugunduzi wa kwanza wa gesi katika ukanda wa bahari ya Hindi ulikuwa ni mwaka 2010, ingawa bado utafiti unaendelea katika hatua mbalimbali. Ripoti ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) imebainisha kuwa mapato yatakayotokana na gesi kwa mwaka inakadiriwa yatakuwa kati ya Dola za Kimarekani bilioni 3 na bilioni 6.

Mwaka 1999, Tanzania ilitangazwa na Benki ya Dunia (WB) kuwa moja ya nchi masikini duniani, jambo ambalo wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanaliita la aibu kwa nchi yenye rasilimali nyingi kama Tanzania kutangazwa kuwa miongoni mwa nchi masikini na zinazohitaji misaada ya hali na mali duniani.

Takwimu zinazopatikana kutoka TPDC zinaonyesha kwamba kati ya futi zaidi ya ujazo wa trilioni 53 za gesi asilia zilizogundulika nchini, ni futi za ujazo za gesi milioni nne hadi nane zinazotumika kwa sasa kwa ajili ya kuzalishia umeme, kupikia pamoja na magari kama mbadala wa mafuta aina ya petroli.

Kwa mujibu wa TPDC, nchi inapoteza takriban Shilingi trilioni 1.6 kila mwaka kutokana na kutumia mafuta ya kuzalisha umeme pamoja na kununua umeme unaozalishwa na makampuni binafsi kulingana na mikataba iliyopo inayolitafuna Taifa. 

Wataalamu wa TPDC wanasema kuwa kiasi cha gesi asilia kinachotumika kwa sasa nchini, ni sawa na asilimia 16 tu ya gesi asilia yote iliyogundulika.

Nchi ya Norway, ambayo kwa sasa ina idadi ya watu wasiozidi milioni tano, inapata neema kubwa kutokana na sekta ya mafuta na gesi asilia. Mfuko ulioundwa kwa ajili ya kuweka fedha za rasilimali hizo katika nchi hiyo, unatajwa kuwa na kiasi cha dola za Marekani bilioni 500, ambazo hata Serikali ya nchi hiyo haijui itazitumia wapi kutokana na wingi wa fedha hizo.

Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, anasema "Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizobarikiwa kuwa na rasiliamali nyingi na kwa hilo tunamshukuru Mungu sana na hizi raslimali lazima zitumike na katika hili ni lazima kushirikiana na nchi nyingine zenye uwezo. Lakini kinachotakiwa lazima zitumike kwa faida ya nchi na watanzania kwanza."

Mh. Sumaye anaongeza kuwa Kampuni za nje zije zichimbe lakini lazima kuwekeana utaratibu mzuri wa Watanzania kufaidika zaidi kuliko wao, na kuongeza kuwa hali hii ipo katika nchi nyingi za Afrika kwasababu bado hatujawa na utaalamu mkubwa katika suala zima la kuwekeana mikataba hii, kwani wataalamu hao wanatuzidi sana. Hivyo Afrika inatubidi tuinuke sana.

"Hivi karibuni nilikuwa katika mkutano World Energy Forum uliofanyika Afrika Kusini ambapo nilikuwa mgeni rasmi katika kufunga mkutano huo na nieleza Afrika tunavyonyonywa sana inatakiwa tukabiliane na hili na tusipokabiliana na hili basi tutaendelea kufaidisha wengine tukidhani ndio utaratibu wa kuendesha biashara hizo," anasema.

Mh. Sumaye anatoa wito wa kuwekeza na kusomesha vijana wetu kupata utalaamu kwenye sekta hizi za gesi, mafuta na madini sambamba na kwenye suala zima la sheria za kimataifa zinazohusika na mambo haya. 

Aidha, amehsauri fedha zinazopatikana kutoka kwenye rasilimali hizi zitumike kuendeleza watu, kuendeleza nchi na miundomnbinu yake na nyingine kwa kadri inavyowezekana kuwekezwa kwa namna ambayo vizazi vijavyo vitafaidika sana kwasababu madini, mafuta ni vitu vinavyokwisha.

"Basi hizo fedha tuwekeze katika utaratibu ambao watoto wetu wanaokuja watazifaidi. Lakini,hatujawa na utaratibu wa kuwekeza fedha kutokana na rasilimali hizi kwa ajili ya vizazi vijavyo.Tunaweza kuona mifano katika nchi kama Uingereza, Norway ambavyo zinafanya hivyo na wanafanikiwa sana," anaeleza.

No comments: