Tuesday, September 23, 2014

MPANGO WA AWAMU YA PILI WA UTEKELEZAJI WA MAENDELEO YA SEKTA YA MAJI WAZINDULIWA TANZANIA

Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Philippe Dongier wakikata utepe kuzindua rasmi Mpango wa Awamu ya Pili ya Utekelezaji wa Maendeleo ya Sekta ya Maji.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Inj. Mbogo Futakamba, akisoma hotuba katika uzinduzi rasmi wa Mpango wa Awamu ya Pili ya Utekelezaji wa Maendeleo ya Sekta ya Maji, akiwa na Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Philippe Dongier.
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe, akisoma hotuba katika uzinduzi wa Mpango wa Awamu ya Pili ya Utekelezaji wa Maendeleo ya Sekta ya Maji.

Baadhi ya Washirika wa Maendeleo wa Tanzania waliohudhuria hafla hiyo.
Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Maji.

Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe,jana amezindua Mpango wa Awamu ya Pili wa Utekelezaji wa Maendeleo ya Sekta ya Maji, kwa kipindi kingine cha miaka 5 kuanzia Julai Mosi, 2014 mpaka Juni 30, 2019 katika Makao Makuu ya Wizara ya Maji, Ubungo baada ya kukamilika kwa Mpango wa Awamu ya Kwanza wa Utekelezaji wa Maendeleo ya Sekta ya Maji.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Washirika wa Maendeleo, Watumishi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Watumishi wa Wizara ya Maji na Taasisi zake.

“Tunapozindua Awamu ya Pili ya Programu hii, tunajivunia mafanikio ya Awamu ya Kwanza katika kuboresha usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji kwa kuanzisha Bodi ya Taifa ya Maji na Bodi za Maji za Mabonde yote 9 nchini zenye wajumbe kutoka sekta mbalimbali.

Na pia, kuzijengea uwezo bodi hizo kwa kuzipatia watumishi pamoja na vitendea kazi katika kuhakikisha zinatekeleza majukumu yake ipasavyo”, alisema Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe.

Aidha, Prof. Maghembe alisema kwamba ili kukabiliana na uharibifu wa vyanzo vya maji unaosababishwa na shughuli za kibinadamu, tumeandaa Programu Maalum ya Miaka 5 ya utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali utakaoanza 2014/15.

Pia, Prof. Maghembe alisema kwamba katika kutekeleza Awamu ya Pili ya Maendeleo ya Sekta ya Maji chini ya utaratibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Wizara imedhamiria kujenga miundombinu ya huduma bora za maji, usafi wa mazingira na vyoo kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi na kuendelea kutoa mafunzo na ushauri kwenye taasisi za umma na kaya zote za mijini na vijijini zijenge vyoo bora na kuzingatia usafi binafsi na mazingira.

Prof. Maghembe aliagiza kwamba zipewe kipaumbele kazi za usimamizi wa miradi inayotekelezwa, ikamilike ndani ya muda uliopangwa kwa mujibu wa mikataba na kuhakikisha kuwa miradi hiyo inalingana na thamani ya fedha iliyotumika.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Philippe Dongier aliipongeza Wizara ya Maji kwa kutekeleza Awamu ya Kwanza ya Programu hii kubwa na kuridhishwa na maendeleo yake mazuri. Pia, alisema kwamba kwa niaba ya Washirika wenzake wa Maendeleo wanapendelea baadhi ya vipaumbele ikiwemo kuweka mpango maalum wa kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa ili kukabiliana na changamoto za uharibifu wa rasilimali za maji kwa ajili ya kupata maji ya kutosha.

Mpango wa Awamu ya Kwanza umefanikiwa kuongeza vituo vya kuchotea maji vijijini, kutoka vituo 44,738 vilivyokuwa vikifanya kazi mwaka 2007 hadi vituo 77,584 mwezi Juni, 2014 ambalo ni ongezeko la asilimia 78 ukilinganisha na lengo la awamu hii, ambalo lilikuwa ni kujenga vituo 41,900.

Vile vile, ongezeko la wateja wapya 236,541 waishio mjini, wenye makazi yenye jumla ya watu 2,700,000 sawa na asilimia 90 kwa kulinganisha na wateja 287,200 waliokuwa wamelengwa, wenye makazi yenye watu 3,000,000.

Mpango wa Utekelezaji wa Maendeleo ya Sekta ya Maji, ni mpango wa miaka 20 unaotekelezwa kwa awamu na ulizinduliwa rasmi na Rais wa Tanzania, Mh. Jakaya Kikwete, Julai Mosi, 2007 na unategemewa kukamilika ifikapo Juni, 2025.

Madhumuni makuu ya Programu hii ni kuhakikisha kuwa Sekta ya Maji inayafikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ifikapo mwaka 2025, yenye dhima ya kuwapatia wakazi wote wa mijini huduma za maji safi na salama na kuwapatia huduma hizo wakazi wa vijijini kwa asilimia 90.

Awamu ya Pili ya Programu hii inakadiriwa kugharimu Dola za Marekani Trilioni 3.34, ambazo zitatokana na Bajeti ya Serikali kwa kuchangiwa na Washirika wa Maendeleo.

No comments: