Thursday, May 23, 2013

Uwazi na Uwajibikaji katika Usimamizi na Matumizi ya Maliasili za Nchi Hukuza Maendeleo


Mojawapo kati ya vipaumbele muhimu vya Marekani nchini Tanzania ni kukuza maendeleo ya kiuchumi na kujenga uwezo (empowerment) wa raia wote kwa ubia na Watanzania kutoka sekta zote. Nchi hii imejaaliwa neema ya kuwa na maliasili nyingi na utajiri mkubwa, mbali na kuwa na vivutio vingi vya dunia kama vile Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama za Taifa na maeneo ya urithi wa Dunia yanayotambuliwa na UNESCO kuanzia Kilwa Kisiwani hadi Zanzibar. Wakati dunia ikitambua hazina hizi kuwa na thamani kwa dunia nzima, bado ukweli ni kuwa, kwa njia ya kipekee kabisa hazina hizi ni za Kitanzania. Pamoja na hali hii, baadhi ya raia wanajiuliza ni kwa namna gani uchumi wa Tanzania utabadilika na kuwa ule wenye kuleta ustawi. 

Mustakabali wa maendeleo ya Tanzania utategemea mawazo na maono ya uongozi wa Watanzania wenyewe. Nimevutiwa sana na jitihada za Watanzania kutoka serikalini na taasisi huru za kiraia kutafuta njia mpya zenye uwazi, uwajibikaji na uadilifu zaidi katika kusimamia na kutumia utajiri mkubwa wa asili ambao nchi hii imejaliwa kwa manufaa ya wote. Mpango wa Kimataifa wa Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia zinazohusika na Uvunaji Maliasili (Extractive Industry Transparency Initiative - EITI)  ni nyenzo inayoweza kusaidia katika kufikia azma hii adhimu na inayostahili kufikiwa kwa haraka .

Yatupasa tutambue kuwa zaidi ya watu bilioni 3.5, takriban nusu ya watu wote duniani, wanaishi katika nchi zilizo na utajiri wa asili kwa mfano mafuta, gesi na madini. Hata hivyo, katika maeneo mengi, utajiri huu hautumiki katika kusaidia mipango ya maendeleo ya mataifa yao au kusaidia kuwakwamua raia kutoka katika lindi la umasikini.  Mojawapo kati ya sababu kuu ya hali hii ni kuwa uvunaji wa rasilimali hizi hutoa changamoto nyingi kwa serikali. Changamoto hizo ni pamoja na ile ya kuhakikisha kuwa uvunaji huo unasimamiwa kamilifu, kwa uwazi na kwa njia inayowahusisha kikamilifu wadau wote. Kutokana na hali hii huu ni wakati mwafaka wa kufikia makubaliano mapana kuhusu viwango vya juu tunavyopaswa kuvifikia katika usimamizi wa rasilimali hizi.

Tarehe 23 na 24 Mei mwaka huu, wawakilishi wa serikali, sekta binafsi na jumuiya huru za kiraia kutoka duniani kote walikutana huko Sydney, Australia kwa ajili ya Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa EITI.  EITI ni mfumo kimataifa ambao serikali kwa hiari yao zenyewe, huahidi kusimamia kwa uwazi na uwajibikaji shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya mafuta, gesi na madini katika nchi zao.  Ni kwa sababu hiyo, Marekani inaelekea kuungana na Tanzania na jumuiya ya mataifa mengine zaidi ya 35 kutoka Afrika, Asia, Marekani ya Kusini na Ulaya ambayo yameonyesha dhamira ya kuwajibika kwa dhati na kwa uwazi kwa watu wao kwa kuwa wanachama kamili wa EITI. 

Kwa kupitia EITI, nchi wanachama hushirikiana na sekta binafsi na asasi za kiraia kuchapisha taarifa ya mwaka ambayo, pamoja na mambo mengine, huonyesha taarifa za mapato ambayo serikali imeyapata pamoja na taarifa za mapato ya makampuni yanayojihusisha na shughuli za uchimbaji na biashara ya mafuta, gesi na madini. Mfumo huu huongeza uwazi, huimarisha uaminifu na kutoa takwimu muhimu zinazohitajika katika kuhakikisha na kufuatilia uwajibikaji.

Marekani imekuwa ikiisaidia EITI toka kuanzishwa kwake zaidi ya miaka kumi iliyopita. Mwezi Desemba 2012,   tulifurahishwa na tangazo kwamba Tanzania imekuwa nchi ya kumi barani Afrika kukidhi viwango vya EITI. Tunapongeza hatua hii kubwa iliyopigwa na Tanzania katika kukuza uwazi na uwajibikaji. Jitihada za Tanzania kujiunga na EITI zilianza mwaka 2009 na kufanikiwa kwake kufanya hivyo katika kipindi cha miaka mitatu tu  kunaonyesha jinsi misingi EITI kuhusu  uwazi katika mapato ilivyo na manufaa kwa nchi zote katika kanda zote na viwango vyote vya maendeleo.

Bunge la Marekani huzitaka baadhi ya kampuni za Kimarekani zinazojihusisha na shughuli za mafuta, gesi na madini kuwasilisha taarifa zao za kila mwaka kwa Tume ya Masoko ya Hisa (U.S. Securities and Exchange Commission) kubainisha malipo mahsusi wanayoyatoa kwa serikali mbalimbali duniani kwa ajili ya shughuli za mafuta, gesi na madini. Taarifa hizi zitajumuishwa na zile za EITI kuonyesha malipo yanayopokelewa na serikali mbalimbali kutokana na maliasili zake, hata kama nchi hizo si wanachama wa EITI. 

Hata hivyo, uwazi katika mapato pekee hautoshi kuwasaidia raia kuona picha ya jumla ya jinsi ambavyo serikali zao zinasimamia rasilimali  yao ya mafuta, gesi na madini. Ni lazima twende mbali zaidi.  Hivyo wiki hii mjini Sydney, wanachama watakubaliana kuhusu mabadiliko kadhaa ya kimkakati katika mpango wa EITI.

Lengo ni kufanya taarifa za EITI kuwa za kina na zenye kuaminika zaidi  na zilizo rahisi kufanyiwa uchambuzi. Aidha, mabadiliko hayo yatazitaka serikali kutoa taarifa muhimu kwa raia wake kuhusu sekta za mafuta, gesi na madini katika nchi zao, ikiwa ni  pamoja na taarifa kuhusu leseni zilizotolewa, makampuni au watu waliopewa leseni hizo, kiasi gani kinazalishwa na nafasi ya makampuni ya mafuta/madini yanayomilikiwa na serikali katika sekta husika. Aidha, EITI itazihimiza serikali kwenda mbali zaidi na kuchapisha kwa hiari yao wenyewe mikataba halisi iliyoingia na makampuni husika.  Utaratibu huu wa uwazi, utakuwa na manufaa kwa Makampuni ya Kimarekani kwa kuyawezesha kuyaelewa vizuri mazingira ya kiutendaji na kibiashara ya nchi husika yanapofikiria kufanya maamuzi kuhusu uwekezaji.

Marekani inaunga mkono mabadiliko haya yatakayowezesha EITI kuwa chombo che ufanisi zaidi katika kuwasaidia raia katika nchi zenye utajiri mkubwa wa maliasili kufaidika kutokana maliasili hizo. Wakiwa na taarifa, wananchi wataweza kuziwajibisha serikali zao hivyo jamii yote kwa ujumla kunufaika kutokana na mapato yatokanayo na rasilimali zake. Kwa kuwa na uwazi na matumizi yenye ufanisi ya maliasili, raia ambao hapo awali walikuwa katika lindi la ufukara nao pia wataweza kuwa na tumaini la kuwa na mstakabali mwema wenye ustawi ambapo wataweza kupata huduma bora za afya, elimu bora na kuweza kutumia uwezo wao kwa kadri ya upeo wao kuchangia katika maendeleo ya Tanzania.

Alfonso E. Lenhardt 
Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

1 comment:

Issangya said...

Makes sense. Thanks Sir!